May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lake Energies, M-Pesa washirikiana kurahisisha malipo kidijitali

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

KAMPUNI ya Lake Energies kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom kupitia huduma yake ya M-Mpesa, wamezindua Kampeni ya malipo ya kidijitali kwa wateja, kulipia mafuta kwa simu katika vituo vyake nchi nzima.

Hayo ameyasema leo na Mkurugenzi wa Operesheni za M-Pesa wa Vodacom, Tito Mbise kwa niaba ya Mkurugenzi wa M-Pesa, wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo jijini Dar es Salaam.

Mbise amesema, hiyo ni sehemu ya mkakati wa M-Pesa kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali kuhakikisha usalama, urahisi, na uwazi katika shughuli za biashara.

“Kupitia ushirikiano huu, mbali na kurahisisha malipo, wateja watarudishiwa 10% ya malipo yao ya mafuta wanapofanya malipo kupitia M-Pesa siku za Ijumaa, Jumamosi, na Jumapili kuanzia msimu huu wa msimu wa sikukuu mpaka mwezi wa Januari.

“Tunaelewa kwamba watu wengi wanasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kuwatembelea jamaa na wapendwa wao wakati huu, hivyo suluhisho hili la malipo ya kidijitali linakuja wakati muafaka kwa sababu watu hawatalazimika kuwa na wasiwasi wa kubeba pesa taslimu ambazo huhatarisha usalama wao,” amesema Mbise.

Mbali na kurudishiwa pesa papo hapo ya kiasi cha 10%, kulipa katika vituo vya Lake Energies kupitia M-Pesa pia itaendelea kuwaongeza wateja nafasi za kushinda zawadi mbalimbali kupitia kampeni inayoendelea ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’.

Amezitaja baadhi ya zawadi ni pesa taslimu, pikipiki, luninga za kisasa, simu janja, na router za 5G.

Hata hivyo Mbise amesema, kwa miaka 15 sasa, M-Pesa ya Vodacom inajivunia mtandao mpana wa wafanyabiashara wapatao 275,000 nchini kote, wanaokubali suluhisho la kulipa kwa M-Pesa.

Amesema, Vodacom ikiwa imejikita katika kurahisisha maisha ya kila siku ya wateja wake, inaendelea kuwa na ubunifu, ambapo hivi karibuni imezindua huduma ya mkopo wa mafuta ‘CHOMOKA’, inayowawezesha madereva kujaza mafuta hata wanapokuwa hawana salio la kutosha barabarani, katika vituo mbalimbali nchini kote.

Kupitia ushirikiano huu, wateja wa M-Pesa wanaweza kunufaika na huduma hii ya mkopo wanaponunua mafuta katika vituo vyote vya Lake Energies.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Rejareja wa Lake Energies Tanzania, Fredy Mchau, amesema dhamira kubwa ya Kampuni hiyo kuhakikisha wateja wanaotembelea vituo vyao wanapata chaguzi mbalimbali za malipo.

“Ushirikiano huu na kampuni inayojitolea kutoa suluhisho za malipo ya kidijitali ni hatua muhimu kuelekea kufikia lengo hili.

“Tunatarajia kunufaika na mtandao mpana wa M-Pesa nchi nzima, ambapo huduma zetu pia zinapatikana,” amesema Mchau.

Mchau amesema, Lake Energies ina vituo 139 kote nchini, lakini wanasaidia juhudi za serikali za kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa kuhamasisha Watanzania wengi kubadilika kwenye malipo na kuacha kubeba pesa taslimu ambayo inaweka usalama wao hatarini.

“Tunahakikisha wateja wote wanaokuja vituoni kwetu kupata huduma sasa wanaweza kulipa kwa M-Pesa,” amesema.

Hata hivyo amesema kwa Kushirikiana na M-Pesa ni sehemu ya mkakati wao wa kutoa huduma na chaguzi bora kwa wateja, wakipigania uchumi usio na pesa taslimu.

“Napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha Lake Energies kwenye familia ya M-Pesa, huduma inayoaminiwa na zaidi ya wateja milioni 17. Uwepo wenu umepanua wigo wa huduma na suluhisho zinazopatikana kwenye jukwaa letu.

“Pamoja, tukienea nchi nzima, bila shaka itakuwa faraja kwa wateja wetu ambao walikuwa wanatarajia kufanya malipo kupitia simu za mkononi lakini hawakuweza,” alihitimisha Mkurugenzi wa Operesheni za M-Pesa wa Vodacom.

Lake Energies, inayojulikana awali kama Lakeoil, ni mtoa huduma mkubwa wa suluhisho za nishati binafsi katika Afrika Mashariki na Kati, na vituo zaidi ya 540 katika eneo hilo, ilianzishwa mwaka 2016, na ni kampuni inayokua kwa kasi zaidi katika sekta ya uuzaji mafuta.