May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yabaini mifumo inayotia asara serikalini

Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Haima Mdee akizungumza Bungeni jijini Dodoma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini kuwepo kwa mifumo dhaifu ya ukusanyaji mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani hali inayosababisha upotevu wa fedha Serikalini.

Akitoa taarifa ya kamati hiyo kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa Fedha ulioishia June 30 2022,Mwenyekiti wa Kamati hiyo Halima Mdee amesema pia halmashauri nyingi zimekosa uthabiti katika ukusanyaji wa madai kutoka kwa wadaiwa mbalimbali .

“Mifumo hii dhaifu inatoa mianya ya uvujaji na upotevu wa fedha za umma na kuzifanya Halmashauri kutofikia malengo yake ya kibajeti hivyo kuongeza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.”

Kufuatia hali hiyo  Bunge limeazimia na kuitaka  Serikali iandae mikataba ya utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato ya ndani itakayokuwa na vigezo  kwa Wakurugenzi wote.  

Aidha amesema,katika kila robo mwaka, kila Katibu Tawala Mkoa afanye tathimini iwapo Wakurugenzi hao wamefikia malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuwasilisha taarifa hiyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  kwa hatua stahiki.

Kamati hiyo imeitaka Ofisi ya Rais Tamisemi na Makatibu Tawala wa Mikoa ihakikishe fedha zote zilizokusanywa kupitia Mashine za kukusanya mapato (POS) Shilingi Bilioni 11.07 zinawasilishwa Benki kabla ya mwezi Aprili, 2024 huku  watendaji wote waliohusishwa wachukuliwe hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa kamati hiyo kila Halmashauri ifanye upya tathimini ya kina juu ya uwezo wa mawakala wa ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha mikataba yote kati ya Halmashauri na Mawakala hao inapitiwa na Mwanasheria wa Halmashauri na hatua za kisheria kwa Mawakala watakaokiuka matakwa ya kimkataba zichukuliwe.

Aidha amesema  Serikali ihakikishe kiasi cha Shilingi Bilioni 37.34 kutoka katika vyanzo muhimu vya mapato ya ndani ya Halmashauri kinakusanywa,kila Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania, wahakikishe wanakuwa na taarifa sahihi kuhusu mauzo ghafi ya wafanyabiashara wote waliosajiliwa katika maeneo yao na kukusanya ushuru wa huduma kwa mujibu wa Sheria.

 Mdee amesema,taarifa ya CAG imebainisha uwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma katika Halmashauri ambapo rasilimali za Umma zimekuwa zikitumika kinyume na Sheria, kanuni, Miongozo na Taratibu  matumizi yasiyofaa ya fedha za umma yamekuwa yakisababisha hasara mbalimbali kwa Halmashauri.

“Hivyo Bunge linaazimia kwamba, Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu watumishi wote waliofanya malipo kwa fedha taslimu kwa kiasi kilichohojiwa cha Shilingi Bilioni 1.51 kinyume cha Mwongozo wa Uhasibu wa Halmashauri wa Mwaka 2021,Serikali ichukue hatua za kinidhamu na kisheria kwa watu wote waliofanya matumizi ya Shilingi Bilioni 11.78 bila ya nyaraka halali za matumizi hayo.”amesema Mdee

Pia Kamati hiyo imeazimia kwamba,Serikali ichukue hatua kwa watumishi wa Halmashauri waliotumia kiasi cha Shilingi Bilioni 7.7 kutoka katika akaunti ya amana kwa matumizi yasiyopangwa na kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa lakini pia Serikali kupitia ofisi ya Rais  TAMISEMI iwaelekeze Makatibu Tawala Mikoa kufuatilia na kuhakikisha watumishi wa Halmashauri zao waliofanya matumizi yasiyo na tija ya Shilingi Milioni 898.85 wanachukuliwa hatua za kinidhamu.

 Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo Halmashauri nyingi zimebainika kutozingatia Sheria ya Ununuzi wa umma Sura 410 na kanuni zake pamoja na uwepo wa dosari katika usimamizi wa mikataba.

Amesema, ukiukwaji wa Sheria hiyo kwa kipindi kirefu umekuwa ukiingiza Serikali katika hasara na fedha nyingi za umma zimekuwa zikipotea katika eneo hili hadi kufikia Shilingi bilioni 106.799.

Kuifuatia amesema Bunge limeazimia  kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ifanye ukaguzi wa kina katika maeneo yote yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG ambayo yameonesha kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ikiwa ni pamoja na matumizi ya force account na kuchukua hatua stahiki kwa watumishi waliohusika na dosari hizo kwa mujibu wa Sheria.

Pia limeazimia Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ihakikishe wanasheria wanapitia mikataba yote iliyohojiwa na CAG ya Shilingi Bilioni 6.68 ambayo haikuhakikiwa na Mwanasheria na kuainisha dosari zilizomo katika mikataba hiyo na hatua stahiki zichukuliwe kwa waliohusika.

“Vile vile, Kwa Mkurugenzi atakayeingia mkataba mpya bila ya kuhakikiwa na mwanasheria, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake na Serikali ihakikishe inalipa madeni ya wakandarasi na wazabuni yenye jumla ya Shilingi Bilioni 7.8 kwa mujibu wa mikataba ya kazi waliyoingia.

“Serikali ihakikishe waliosababisha hasara kwa kufanya ununuzi wa vifaa vya ujenzi zaidi ya mahitaji kama ilivyoainishwa katika Ripoti Kuu ya CAG wanachukuliwa hatua za Kisheria na kuhakikisha hasara hiyo inafidiwa,

“Serikali ihakikishe bidhaa zilizolipiwa kabla ya kupokelewa za Shilingi Bilioni 3.29 zinapokelewa na kuhakikiwa kwa mujibu wa mikataba; na f) Serikali ichukue hatua stahiki kwa Wakurugenzi waliofanya ununuzi wa Shilingi Bilioni 7.45 bila ya kutumia njia ya 92 ushindanishi wa bei na kusababisha dosari kadhaa katika ununuzi uliofanyika. “amesisitiza Mdee

Kuhusu uendeshaji usiofaa wa Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mdee amesema,kumekuwepo kwa kutozingatiwa kwa kanuni za usimamizi na utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema, ukiukwaji wa Kanuni hiyo umesababisha lengo la utoaji wa mikopo hiyo kwa jamii lisifikiwe huku akisema azimio la Bunge katika eneo hilo ni pamoja na kila Halmashauri ichangie Asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwenye Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu na kuhakikisha kiasi kilichohojiwa cha Shilingi Bilioni 5.06 kinapelekwa katika mfuko huo.

Pia Bunge limeazimia Wakurugenzi wahakikishe kiasi cha Shilingi Bilioni 88.42 kilichokopeshwa katika vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kinakusanywa kabla ya mwezi Juni, 2024.

Aidha Bunge limesema kuwa pindi utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo utakapoanza tena, Serikali ihakikishe mikopo hiyo inatolewa kwa kuzingatia uwiano uliowekwa kisheri wa 4:4:2; lakini pia  Serikali ihakikishe Halmashauri ambazo zilitoa mikopo kwa Vikundi vilivyositisha shughuli za Biashara na kushindwa kurejesha Shilingi Bilioni 2.25 pamoja na Halmashauri zilizotoa mikopo kwa vikundi ambavyo havikupatikana kwa ajili ya uhakiki (Vikundi hewa) vyenye Shilingi Milioni 895.94 zinafanya ufuatiliaji wa kina na kuhakikisha fedha hizo zinakusanywa.