May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Dar aridhishwa na uzalishaji umeme Kinyerezi

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameridhishwa na kituo cha ufuaji umeme cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam, jinsi kinavyofanya kazi ili wananchi waweze kupata huduma ya umeme kirahisi.

Hayo ameyasema leo, na Mkuu wa Mkoa huyo alipotembelea Mitambo ya kufua umeme Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II, jijini Dar es Salaam.

Chalamila amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika miradi hiyo kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na hadha ya umeme.

“Nimeridhishwa na jinsi mitambo ya kufua umeme hapa Kinyerezi inavyoendeshwa, kwani naamini baada ya muda kero za umeme tutazisikia kwenye bomba.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda wananchi wake ndio maana anafanya kila liwezekano kuhakikisha kero za umeme hapa nchini zinatoweka,” amesema Chalamila.

Katika hatua nyingine, Chalamila amewataka wananchi kutunza mazingira ili kupata vyanzo vya maji na ili siku moja matumizi ya gesi kwa ajili ya umeme yaweze kupungua ambapo kwa sasa uzalishaji aslimia kubwa utegemea gesi.

Naye Meneja wa miradi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Didas Lyamuya amesisitiza kuwa Watanzania wanatakiwa kutunza mazingira ili kupata vyanzo vya maji ambayo vinaweza kuzalisha umeme kwa wingi.

Amesema Serikali imewekeza kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika hivyo kutokana na mitambo ambayo wataifunga tatizo la umeme kwa wakazi waliowazunguka hawapata shida.

“Umeme huu ni wagesi hivyo ili tuondokane na hali hiyo wananchi hawana budi kutunza vyanzo vya maji ikiwemo mifereje, kwa hiyo kila mmoja anatakiwa kutoa taarifa kwa wenyeviti wa mitaa iwapo kuna taarifa ya kuiharibu miferji hiyo,” amesema Lyamuya.

Amemshukuru Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila kwa kufanya ziara kwenye mitambo hiyo ya ufuaji Umeme Kinyerezi na kujionea mwenyewe pamoja na kuridhishwa na utendaji wake wa kazi

Kwa upande wake Meneja wa kituo cha Kinyerezi I Extension, Marco Zacharia amesema mradi wa Kinyerezi I unazalisha Megawati 150 ambao umegharimu takribani dola za Kimarekani milioni 183 sawa na fedha za Kitanzania shilingi bilioni 402.6.

Amesema, mradi huo uligharamiwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

“Uwezo wa kituo ni kuzalisha Megawati 150. Umeme unaozalishwa hapa kituoni hukuzwa kutoka 11KV kwenda 220KV kisha kusafirishwa kwenye grid ya Taifa kupitia njia nne ambazo ni, Morogoro-220KV, Ubungo-220 KV, Pugu-220KV na Gongolamboto-132KV,” amesema Zacharia.