May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lushanga mbaroni tuhuma za kusababisha ajali

Na Daud Magesa, Timesmajira Online Mwanza

MKAZI wa Mwatulole mkoani Geita, Noel Lushanga (34), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza,kwa kusababisha ajali na majeruhi wawili baada ya gari alilokuwa akiliendesha kuligonga gari jingine.

Ajali hiyo imetokea Mei Mosi,mwaka huu, majira ya saa 2:40 usiku barabara ya Mwanza-Shinyanga, eneo la Mawe Matatu, Kata ya Usagara,wilayani Misungwi.

Akizungumza tukio hilo Mei 2,mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Naibu Kamishna wa Polisi,Wilbrod Mutafungwa,amesema kuwa Lushanga wakati akiendesha basi la abiria lenye namba za usajili T 669 DEE,aina ya Higher,akitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam, aliligonga gari lenye namba T858 DHE,aina Toyota Hiace linalofanya safari zake kati ya Nyashishi wilayani Misungwi na Ngudu, Kwimba.

Mutafungwa amesema dereva huyo alisababisha ajali wakati akilipita gari la mbele yake bila tadhahari hivyo kuigonga Hiace ilivyokuwa ikiendeshwa na Isaka Bakari(32), mkazi wa Buhongwa wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

Amesema baada ya kugongwa kwa gari hilo dogo alisababisha majeruhi kwa abiria wawili waliokuwa ndani ya hiace hiyo na kuwataja ni Elias David (33),mkazi wa Igoma na Yazidi Swahibu (44),mkazi wa Isamilo wote wa wilayani Nyamagana.

“Abiria hao wote wamepata majeraha usoni na wamepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure,”amesema.

Aidha, Mutafungwa amesema ajali nyingine imetokea huko Kata ya Misungwi wilayani humo,katika stendi ya mabasi,Aprili 30, mwaka huu majira ya saa 1:10 asubuhi,madereva wawili wa pikipiki za bodaboda, wamejeruhiwa baada ya kugongana na kusababisha moto kulipuka.

Amesema Juma Kiselaja (33),mkazi wa Kitangiri wilayani Ilemela akiendesha pikipiki namba MC 600 DNP aina ya Kinglion,, aliigonga pikipiki yenye namba MC 949 DWW aina ya Sanlg iliyokuwa ikiendeshwa na Amos Robert (23), mkazi wa Misungwi.

“Robert akitoka barabara ndogo,aliingia barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga bila tahadhari na kugongwa na bodaboda mwenzake,wote wamepata majeraha yaliyosababishwa na moto uliozuka baada ya ajali kutokea lakini ulizimwa kwa juhudi za wananchi,”amesema Mutafungwa.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Amos Robert ambaye alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi huku Juma Kiselaja akipelekwa kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando.