July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa aipongeza Tanga UWASA

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 Sahili Nyanzabara Geraruma ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga Uwasa) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanawapatia maji safi wananchi na hivyo kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa aliyasema hayo leo wakati alipotembelea mradi wa uendelezaji wa Miundombinu ya Maji Safi ikiwemo kushiriki kuwaunganishia huduma ya maji safi wakazi wa Kata ya Maweni wawili ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa maunganisho ya maji safi kwa mradi huo.

Aidha alisema kwamba wametembelea mradi huo na kuona namna mamlaka hiyo ilivyofanya kazi nzuri kwa ubunifu mkubwa na miradi wanayotekeleza ya kuhakikisha wanawapatia huduma ya maji wakazi wa jiji la Tanga.

“Nalisema hili wazi kabisa bila kusitasita niwapongeze Tanga Uwasa kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhakikisha mnapaelekea wananchi maji huduma ambayo ni muhimu kwa ustawi wa maisha yao ya kila siku hivyo hakikisheni wananchi wanapolipia huduma hiyo wanaipata kwa wakati ”Alisema

Kiongozi huyo aliitaka mamlaka hiyo kuhakikisha wanafikisha maji kwa haraka kwa wananchi ikiwemo kutekeleza majukumu yao kwa wakati pamoja na wananchi wanapolipia waweze kuunganishiwa kwa muda muafaka ili kuepusha malalamiko yasiyokuwa na tija.

“Ndugu zangu watumishi kama wakati mwengine kuna changamoto muwe mnawaeleza wananchi badala ya kusubiri mpaka walalamike na kuilaumu serikali hii “Alisema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge.

Sambamba na hayo aliwakumbusha wananchi kuhakikisha wanajiandaa na kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi kwani ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Violet Kazumba alisema kwamba mamlaka hiyo inatekeleza mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya maji safi katika Jiji la Tanga kupitia Fedha za Uviko zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19.

Mhandisi Violet alisema mamlaka hiyo imeweza kusimamia mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya maji safi Tanga unaogharimu kiasi cha Sh.512,832,602.80 hadi kukamilika wenye urefu wa kilomita 17,640 katika maeneo ya MSD (Mita 4,000),Kichangani-Mji Mwema (Mita 5,125) Mwahako Neema (Mita 3,000),Masiwani Mbugani (Mita 3,300) na Pongwe kusini (Mita 2,215).

Aidha alisema katika utekelezaji wa mradi huo ulioanza Novemba 2021 na kukamilika Mei 17,2022 ambapo kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na upanuzi na ununuzi wa mabomba ya urefu wa mita 17,640,Ujenzi wa Chemba 46 na usimikaji wa alama 353 za kuonesha miundombinu ya maji ambapo kazi zote zimekamilika kwa asilimia 100 na fedha iliyolipwa ni Sh.Milioni 468,366,302 sawa na asilimia 84.