April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango wa kukabili maafa wazinduliwa

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam

KAMATI  za uratibu wa Maafa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji zimetakiwa kutekeleza majukumu yake  kikamilifu katika kuzuia, kupunguza vihatarishi na kuwa tayari kukabiliana na maafa  ili kuleta maendeleo  endelevu kwa Wananchi.

Hayo yamesemwa jana  na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt. John Jingu wakati wa hafla ya kushuhudia utiaji saini na kukabidhi Mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa pamoja na Mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa iliyofanyika katika  Halmashauri Wilayani Rufiji moani Pwani.

Amesema kuwa jamii ya Rufiji imekuwa ikihitaji muitikio mkubwa wa Serikali na wadau katika usimamizi kutokana uwepo wa majanga ya maafuriko, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ukame, magonjwa ya mlipuko, wanyama pori pamoja na wadudu waharibifu.

“Ni lazima tuchukue hatua za makusudi za kuzuia na kupunguza vihatarishi na kuwa tayari muda wote katika kukabili maafa yale ambayo hayazuiliki kwa kuwa ni mpango madhubuti ili kuleta maendeleo endelevu,” Amesema Mkurugenzi huyo.

Pia  ametoa shukurani kwa Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) kwa ufadhili wa kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa mpango wa kujiandaa kukabiliana na maafa katika bajeti kwa Halmashauri mbalimbali Nchini.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji,John  Kayombo amebainisha kuwa  Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imechukua hatua za kuandaa mpango wa kujiandaa na kukabili maafa baada ya kufanikiwa kufanya tathimini ya vihatarishi.

 “Halmashauri  inashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu  na imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuandaa mpango wa kijiandaa na kukabili maafa wa Wilaya  kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia madhara hivyo mpango huu utasaidia kuongeza ufanisi ii tuokoe maisha ya wananchi na mali zao,” amesema Kayombo.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Meja Edward Gowele ameahidi kutekeleza mpango huo kwa kushirikiana na kamati, kusimamia na  kuufanyia kazi mpango huo.