Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MCHAMBUZI wa masuala ya kisiasa nchini, Deus Kibamba, amesema haoni dhamira ya dhati ya viongozi wa serikali ya kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya kwa wakati. Amesema katika siku za karibuni kumekuwa na kauli zinazozungumzia maboresho ya katiba badala ya kuandikwa kwa katiba mpya.
Kibamba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mjadala kuhusu fursa za kimataifa na kikanda katika nafasi za kiraia na ulinzi wa haki za binadamu.
“Binafsi ukiniuliza suala la kupata katiba mpya, ambayo ndiyo msingi wa changamoto nyingi kwenye jamii, sioni dhamira ya dhati ya viongozi na hivyo, asasi za kiraia na wananchi lazima tuungane ili kupata katiba Mpya.”amesema Kibamba

Katika mjadala huo, Wakili Jebra Kambole, Wakili PraiseGod Joseph na James Marenga wamezungumzia nafasi ya ushirikiano na vyombo vya kimataifa na kikanda katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusu haki na utawala wa sheria nchini.
Wakili Jebra Kambole amesema kesi za maslahi ya umma zilizofunguliwa na baadhi kushinda zimekuwa na manufaa makubwa, ikiwemo kuchochea kurejea kwa uwajibikaji na kuimarisha utawala wa sheria.
Kwa upande wake, James Marenga amesema kumekuwa na jitihada za kisheria zinazolenga maboresho ya sheria, lakini changamoto inaendelea kujitokeza pale serikali inaposhindwa kutekeleza baadhi ya maamuzi ya mahakama.

Mjadala huo wa wadau kuhusu mikakati ya utetezi wa utawala wa sheria, nafasi ya kiraia na marekebisho ya sheria nchini umeandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chama cha Mawakili Afrika Mashariki, Chama cha Mawakili Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Mawakili wa Pan Afrika (PALU).
Mkutano huo umefanyika chini ya mradi wa Kulinda Utawala wa Sheria, Nafasi ya Kiraia na Uwajibikaji Tanzania kupitia Ushirikiano na Ubia Ulioboreshwa (SCATZ), unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya.

More Stories
Kapinga apongeza uongezaji thamani kiwanda cha mafuta
Mbeya yapokea magari mapya
Wajenga nyumba ya watumishi kwa mapato ya ndani