April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kambi ya riadha yaahidi medali, kuondoka nchini Agosti 3

Na Mwandishi Wetun TimesMajira Online

NYOTA wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Riadha ya Tanzania wameendelea kujifua jijini Arusha kuelekea kwenye mashindano ya Olimpiki 2020/2021 yatakayoanza kutimua vumbi Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka huu katika jiji ya Tokyo nchini Japan.

Kambi hiyo ya Olimpiki inaundwa na wachezaji mbalimbali wakiwemo Alphonce Simbu, Gabriel Geay na Failuna Matanga waliofuzu kushiriki mashindano hayo pamoja na wakimbiaji wengine ambao wanafanya pamoja mazoezi.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) Silas Isangi, ameuambia Mtandao huu kuwa, hadi sasa nyota hao wanaendelea vizuri na mazoezi yao na kile wanachokionesha kinawapa imani kubwa kuwa wataweza kurudi hapa nyumbani na medali.

Amesema, kwa sasa morali yao ipo juu sana ukilinganisha na awali walipoingia kambini na hiyo yote inatokana na mashindano mbalimbali ya ndani ya riadha ambayo walishiriki na kufanikiwa kushinda.

Pia Watanzania wanatakiwa kutegemea makubwa kutoka kwa nyota hao kwani kwa muda uliobaki wa maandalizi wana imani watakuwa bora zaidi na hawahataweza kuwaangusha kwani wanakwenda kwa ajili ya kushindana na si kushiriki.

“Morali inayooneshwa na nyota wetu inatupa imani kubwa kuwa wataweza kufanya vizuri na kurudi nyumbani na medali kwani hata sasa wanachokisema ni kuwa wanakwenda kwenye mashindano hayo makubwa dunia kwa ajili ya kuipeperusha vema bendera ya nchi hivyo watahakikisha hawaendi kwa ajili ya kushiriki bali kupambana kutwaa medali,” amesema Isangi.

Amesema kuwa, kuelekea kwenye michiano hiyo, timu hiyo ya Taifa itaondoka Agosti 3 kwani watakimbua Agosti 8.

Pia amesema, awali walipanga kikosi hicho kuondoka Juni 29 kwa ajili ya kambi ya mwisho ambayo walipanga kuiweka kwenye mji na Nagai lakini baada ya kutapa taarifa ya hali yake ya hewa wameona ni bora kufanya mabadiliko hayo.

“Awali tulipanga kambi yetu ya mwisho iwe Nagai lakini tililazimika kubadili kutokana na hali ya hewa hivyo wangeenda tarehe 29 wakati wao wanakimbia Agosti 8 ingewapa tabu hivyo wataendelea na kambi yao hapa hapa nchini hadi pale watakapoondoka,” amesema rais Isangi.

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Alphonce Simbu amesema hadi sasa maandalizi yao yanakwenda vizuri na wanaimani kubwa ya kwenda kufanya makubwa katika michuano hiyo ya Olimpiki.

Amesema, nia yao ni kwenda kuipeperusha vema bendera ya Taifa hivyo hawana mzaha hata kidogo katika maandalizi kwani wanachokihitaji ni kutimiza ahadi yao waliyoiweka kwa watanzania ya kurudi hapa nchini na medali.