May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya kudumu ya Miundombinu yaipongeza serikali kwa miradi ya TMA

Na Penina Malundo, timesmajira

KAMATI ya Kudumu ya Miundombinu ya Bunge imeipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta hali ya hewa nchini wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na TMA ikiwemo rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso wakati wa majumuisho ya ziara hiyo mwishoni mwa wiki kwa kuridhishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kupelekea nchi ya Tanzania kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kuihakikishia nchi uhakika wa huduma inayotolewa kwa manufaa ya Taifa letu.

Aidha, Kamati hiyo iliipongeza TMA kwa kuongeza ubora na usahihi wa utabiri ikiwemo wa mvua zilizoambatana na Elnino.Katika hatua nyingine, Kakoso aliagiza uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ufanyike pamoja na maslahi bora ya watumishi.

“Tunaiomba Serikali imarisheni Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ili kiweze kuandaa wataalamu watakaofanya kazi, pili lindeni wafanyakazi wa TMA kwa kuwapatia maslahi mazuri, msipofanya hivyo Serikali itakuwa inasomesha vijana wengi na baadaye wote wanaondoka kwasababu hawalipwi vizuri”,amesema Kakoso.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la KImataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a ameshukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha TMA kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

“Rada hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga ziwani,hali mbaya ya hewa,upepo mkali na kutoa tahadhari kwa wananchi hususani watumiaji wa ziwa Viktoria na kuboresha taarifa zinazotolewa na kuimairisha tija na usalama kwa watumiaji wengine wa taarifa za hali ya hewa kama sekta ya usafiri wa anga, ulinzi, kilimo,uvuvi na utunzaji wa misitu”. Ameeleza Dkt. Changa.

Amesema rada ya hali ya hewa iliyopo Mwanza, inauwezo wa kufanya uangazi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga,Kagera, Mara na eneo kubwa la ziwa vicktoria.

Amesema rada hii ni moja ya uwekezaji mkubwa unaoendelea wa kukamilisha mtandao wa rada saba zenye teknolojia ya kisasa hapa nchini, ambapo rada tano zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya na Kigoma na rada mbili zitakazofungwa Kilimanjaro na Dodoma zikiendelea na mategenezo Marekani.