May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar ashuhudia fainali mashindano ya kuhifadhi qur-an

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, Leo Machi 17, 2024, alikuwa Mgeni Rasmi wa Fainali ya  Mashindano Makuu ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu ya hapa Visiwani.

Fainali ya Mashindano hayo Makuu ya Kimataifa, imefanyika katika Msikiti wa  Jamiu Zinjibar, Mazizini Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, na Kujumuisha Washiriki takriban 12 kutoka  Mataifa ya Afrika Mashariki, Kati na Magharibi, zikiwemo Nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Nigeria, Chad, Ivory Coast, Rwanda, Comoro, Niger na Kenya.

Katika Nasaha zake kwa Hadhira hiyo na wananchi kwa ujumla,Othman ameshukuru Juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya za Kuhifadhisha Qur-an hapa Nchini, kwa Malezi Muhimu ya Vijana, ambayo ni Mchango mkubwa katika Ustawi bora wa Taifa.

Amesema kuwa Malezi yanayozingatia Misingi inayotokana na Kitabu Kitukufu, yanathibitisha heshima, thamani na utukufu wa mwanadamu ulimwenguni.

Alhaj Othman amesema kuwa kwa yeyote anayejali na kuzingatia umuhimu wa Kitabu Kitukufu, anaelewa kwamba huo ni Msingi imara katika ujenzi wa Jamii iliyo bora naambayo imetengenea.

Hivyo amesema, “kutokana na ukweli kwamba Qur-an ni amana kutoka kwa Muumba”, ni wajibu wa kila mmoja  mmoja katika jamii kuitekeleza na kuiishi, kwa kuifuata kikamilifu Miongozo iliyomo ndani yake.

Mheshimiwa Othman  amesema, “Malezi ya Vijana hao wakiwemo hawa ambao wamechuana kuihifidhi Qur-an Leo ni sawa na mbegu bora inayohitaji kukuzwa ili kutoa matunda mema zaidi”.

Vijana hao wa Umri wa takriban kati ya Miaka 16 na 22 wamechuana vikali katika Kuihifadhi Qur-an Tukufu kupitia Njia za ‘Hifdhi’ na ‘Tashjii’, ambapo Mshindi wa Jumla ni Mahamat Hassan Bachar (20) kutoka Nchini Chad.

Mshindi huyo ambaye amepata Alama 98.75 amejinyakulia Kitita cha Shilingi za Kitanzania Milioni Sita (6,000,000) akifuatiwa na Mshindi wa Pili, Abubakar Hassan Muhammad (20) wa Nigeria, aliyepata Milioni 5 (5,000,000) kwa Alama 98.0 , huku Mshindi wa Tatu, Abdinassir Ali Abdi (22) kutoka Kenya, akipata Alama 97.50 na Shilingi Milioni Nne (4,000,000).

Washindi hao, pamoja na Washiriki wenzao wote wa Hatua hiyo, wamejipatia Zawadi nyengine Maalum, Vyeti, na Idhini ya kushiriki Mashindano mengine ya Kimataifa yanayoandaliwa na Jumuiya hiyo.

Kwa upande wa “Tashjii”,  Nassir Rashid Seif wa Zanzibar  ameibuka Mshindi wa Kwanza kwa kujizolea Alama 99.0 na Shilingi Milioni Tatu na Laki Tano (3,500,000), kwa kumshinda Mohamed Khamis Mohamed, pia wa Zanzibar, aliyejipatia Alama 98.0 na pesa taslim Shilingi Milioni Tatu (3,000,000). 

Amiri wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-an Zanzibar, Sheikh Suleiman Omar Ahmad, amebainisha kuwa jumla ya Shilingi Milioni 29 (29,000,000) taslim, zimetolewa kwa Washindi, sambamba na “chochote” kwaajili ya Washiriki wote 12 wa Ngazi ya Fainali ya Mashindano hayo.

Katika Salamu zake, wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Amir wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-an Zanzibar, Sheikh Muhammad Alawy, amesema Lengo la Msingi la Harakati hiyo, ni Kuilea Jamii kwa kufuata Misingi Imara ya Kitabu hicho Kitukufu.

Amefahamisha kuwa Jumuiya yake inaamini kwamba Lengo hilo linatekelezeka kupitia Mashirikiano ya Jamii yote, kuanzia Serikali, Jamii na hadi Familia, pindipo kutakuwepo Mikakati ya Makusudi ya Malenzi na Ulinzi wa Mtoto, tangu anapozaliwa mpaka kufikia utu uzima, na katika nyanja zote za maisha.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mashindano hayo  Sheikh Muhammad Mshenga Matano, kwa niaba ya Majaji wenzake amesema, Mwaka huu umeshuhudia ‘Mchuano Mkali’ kutokana hamasa na maandalizi bora ya Vijana hao, kwa kulinganisha na Misimu iliyopita.

Masheikh, Wanachuoni, na Viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali, wamehudhuria katika Mashindano hayo,  wakiwemo kutoka Taasisi za Kiislamu za Kitaifa na Kimataifa, wakiongozwa Mufti Wakuu wa Zanzibar na Kenya, Sheikh Saleh Omar Kaabi, na Sayyid Ahmad Badawy Jamalillayl Mwinyi-Baba.

Mashindano hayo yanayofanyika kila Mwaka, chini ya Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur-an ya  Zanzibar, yalianza rasmi Machi 12, 2024, kwa Washiriki Wanaume na Wanawake, katika Ngazi ya Mtoano, hapo Msikiti Arafa na Ukumbi wa ‘The Palm’, kabla ya Hatua ya Mchujo wa Kimataifa (Tazkiyah) mnamo Alhamis ya Wiki hii, huko Masjid Fatma, Msikiti uliopo Kihinani, pia Mjini hapa, hatua ambayo ilipekea kupatikana Washindi ambao wamechuana katika Fainali ya Leo.

Hatua hiyo ya Fainali, ya Mashindano hayo kwa Upande wa Wanawake, ilifanyika hapo jana katika Ukumbi wa Piccadily Kombeni, Mkoa wa Mjini- Magharibi Unguja, Mbele ya Mgeni Rasmi, Hajjat Salma Swaleh kutoka Nchini Kenya.

Mashindano hayo  ambayo ni ya 32 tangu kuasisiwa kwa Jumuiya hiyo mnamo Mwaka 1992, kwa mara hii yamebeba Kaulimbiu isemayo, “QUR-AN NDIYO DIRA YA MAISHA YETU”.