April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Julio: Mbinu zitatubeba kwa Sudan Kusini, wachezaji wataka kombe

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, ‘Ngorongoro Heroes’, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameapa kutoa dozi katika mchezo wao wa leo wa Nusu Fainali wa michuano ya CECAFA utakaochezwa kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu dhidi ya wapinzani wao Sudan Kusini ili kutinga hatua ya Fainali.

Tanzania itaingia katika mchezo huo huku ikitaka kuendeleza rekodi nzuri waliyopita kwenye michuano hiyo toka ilipoanza ambapo walipata ushindi wa goli 6-1 dhidi ya Djibouti na kisha wakamfunga Somalia goli 8-1 lakini pia wakitaka kuendelea kuweka rokodi ya kuwa timu inayofunga goli nyingi katika kila mchezo.

Hadi sasa katika michuano hiyo, Nahodha Kelvin John amefunga ‘hat trick’ katika mchezo dhidi ya Somalia ikiwa ni ya pili kufungwa katika michuano hiyo ambapo ile ya kwanza ilipatikana katika mchezo dhidi ya Djibouti iliyofungwa na Abdul Hamis.

Julio amesema, wataingia katika mchezo huo kucheza kufa na kupona ili kupata ushindi ambao utawapeleka katika malengo yao ya kucheza fainalia na kuubakiza ubingwa wa michuano hiyo hapa nyumbani.

Amesema, wanatambua kuwa mchezo huo ni mgumu na wapinzani wao ni miongoni mwa timu bora lakini ameshawaandaa wachezaji wake kisaikolojia na kimbinu ili kuhakikisha wanachukua ushindi dhidi ya Sudan Kusini.

“Benchi letu lilikuwa na kazi kubwa ya kuwaandaa vijana wetu kwa zaidi ya mwezi na nusu na leo tunaingia katika mchezo wa Nusu Fainali kupambana kufa na kupona ili kupata ushindi. Wachezaji wangu wapo vizuri kimwili na kiakili kupambana ili kupata ushindi utakaotupeleka pale tunapopataka,” amesema Julio.

Amesema anaamini kuwa vijana wake hawatawaangusha Watanzania kwani watafanya kazi nzuri na kuwapa Watanzania kile wanachokitarajia kikubwa ni wao kuungana nao katika maombi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) Oscar Mirambo amesema, benchi la ufundi limefanya kazi kubwa ya kutatua changamoto walizoziona katika mechi zao mbili zilizopita ili wasizirudie katika mchezo wao wa leo.

Jambo zuri kwao ni kuwa, vijana wao wanafahamu kuwa katika mchezo huo ni lazima mmoja afungwe na sio kuwa sare itaamua matokeo hivyo kwa namna hiyo wataweza kupambana ili kufanikisha jambo hilo.

“Leo kikubwa tunachotarajia kuona kwa vijana ni mchezo mzuri kwani wanatambua kuwa leo kutakuwa na mshindi ambaye ataenda fainali na atakayeshindwa na kitu pekee kitakachowabeba ni uamuzi na kujituma uwanjani hivyo leo tunatarajia kuona mchezo mzuri ambao utatupeleka fainali, ” amesema Mirambo.

Mkurugenzi huyo amesema, kwa sasa maono ya TFF ni kutaka nchi kuwa Taifa kubwa kwenye medani za soka na ili kufanikisha hilio basi ni lazima kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa na kufanya vizuri.

“Ikiwa vijana watafanikiwa kwenye hili basi tutakuwa tunaishi na kulipa deni
ambalo tumekopeshwa na Watanzania wanaoamini kuwa tunaweza kabisa kupiga hatua
hivyo ni jambo la kumuomba Mungu sana ili kufika tunapotakata,” amesema Mirambo.

Mchezaji wa hiyo, David Kameta amesema kuwa, tayari wameshamaliza maandalizi yote na watahakikisha wanaingia uwanjani kupambana kufa na kupona ili kutimiza kile walichowaahidi Watanzania.

Amesema kuwa, wachezaji wote wana morali kubwa kuelekea kwenye mchezo huo kwani kiu yao ni kuchukua ubingwa wa mashindano hayo na kuubakiza hapa nchini na wanaamini watafanikisha jambo hilo.

Mchezo huo wa Nusu Fainali kati ya Tanzania na Sudan Kusini utatanguliwa na mchezo kati ya Uganda na Kenya ambapo washindi watakutana kwenye Fainali itakayochezwa Desemba 2 ambapo mshindi wa kwanza na wa pili wataziwakisha nchi zao katika Fainali za U-20 za Afrika zitakazofanyia nchini Mauritania