April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kutowaficha watu wenye ulemavu wakati wa sensa ya watu na makazi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi 2022 Anna Makinda ameitaka jamii kutowaficha watu wenye ulemavu wakati wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ili wahesabiwe na kuingizwa kwenye mipango ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kuitaka jamii kuacha kulihusisha zoezi hilo na imani potofu.

Pia amesema sensa ya mwaka 2022 itakuwa shirikishi na itaanzia ngazi ya vitongoji hivyo viongozi wa vitongoji vyote lazima watambue umuhimu wa zoezi hilo.

Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Anna Makinda ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akikagua maeneo ya kuhesabia watu Tanga.

Makinda amesema watu wenye mahitaji maalumu kama walemsvu nao wanatakiwa wahesabiwe huku akiitaka jamii kuachana na tabia ya kuwaficha watu hao kwa kuwa ni sehemu ya idadi ya watanzania.

Aliwataka viongozi wa mitaa na vitongoji kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye zoezi hilo ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za uhakika za idadi ya makundi ya watu kwenye maeneo yao ya uongozi.

Makinda amesema mpango wa sasa wa kuwatumia viongozi wa mitaa na vitiongoji utasaidia kupata taarifa za uhakika kuunga mkono mpango wa serikali wa kuwa na idadi ya watu na mahitaji yao kwa maendeleo yao na Taifa lao.

“Serikali lazima ijue kila wakati kuwa watu wake wakoje ili inapopelekea maendeleo yaende kulingana na idadi ya watu waliopo na tuweze kujenga uchumi uliochangamka lakini pia wananchi oneni umuhimu wa kushiriki zoezi hilo kwa maendeleo ya ustawi wa Taifa letu,”alisistiza Makinda.

Kwa upande wake Msimamizi wa Maandalizi ya Sensa Mkoa wa Tanga,Tumaini Komba amesema kwa upande wa mkoa wa Tanga maandalizi ya kutenda maeneo kwa ajili ya mpango wa kuhesabu watu yameenda vizuri.

Komba alisema isipokuwa walipata changamoto kidogo kwenye wilaya ya Lushoto kutokana na Geografia ya milima na kwamba baada ya kubaini hiyo waliongeza nguvu kutoka kwenye timu nyingine zilizokuwa zimemaliza kazi hiyo kwenye maeneo mengine.

Zoezi la kuhesabu watu litafanyika mwezi Agost Mwaka huu 2022 na kwamba lengo la kutenga maeneo ya kuhesabu watu linalenga kuhakikisha kila karani anajua mipaka ya eneo lake kuepuka kuhesabu watu ambao walishahesabiwa na karani mwingine.