April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Nombo:Kituo cha Umahiri Arusha kuifungwa mitambo ya kisasa

Na WyEST Arusha

Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kuanza ujenzi wa majengo mapya katika kituo chake cha Umahiri cha Nishati Jadidifu Kilicho chini ya Chuo cha Ufundi Arusha  kitakachokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 650 kwa wakati mmoja.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu iliyopo sasa katika kituo hicho  jana Jijini Arusha  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carloyne Nombo amesema ujenzi huo umefadhiliwa na Mradi wa EASTRIP  na unaolenga kuongeza fursa za mafunzo ya Mafundi wenye ujuzi na Stadi katika fani ya Umeme ambapo amesema  miundombinu iliyopo ni ya zamani iliyojengwa na wajerumani miaka ya1930 na haitoshelezi pamoja na Chuo kwamba kiliendelea kutoa mafunzo.   

Prof. Nombo amesema kituo hicho kupitia mradi pia kitawekekwa  vifaa na mitambo mipya ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia ili kiweze kutoa mafunzo yanayoendana na teknolojia ya kisasa na kuzalisha wataalam watakaoweza kushindani katika soko la ajira.

“Hiki kituo kilijengwa miaka 1930 na wajerumani kwa hiyo kina mitambo ya teknolojia ya kizamani kwa hiyo tunakijenga upya ili kiwe na uwezo wa kutoa mafunzo yanayoenda na ukuaji wa teknolojia, pia kiweze kusaidia katika kuzalisha wataalam watakaoshiriki katika kufanya kazi katika miradi ya kimkakati kama katika bwawa la Mwalimu Nyerere” amesema Prof. Nombo.

Aidha, Prof. Nombo amekitaka Chuo cha Ufundi Arusha kuhakikisha kinatekeleza agizo la serikali la kuzalisha vijana wenye ujuzi na umahiri katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupata wataalam watakaoshiriki katika miradi ya kimkakati.

Katibu Mkuu huyo amesema Chuo kinapaswa kutambua kuwa kina deni la kuandaa wataalam hao kwa kuwa tayari miradi imeshaanza ikiwemo ule wa bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linawahitaji.

Naye Msanifu majengo wa kampuni ya Y & P Architects (T) limited Mringo Yassin aliyepewa jukumu la kubuni michoro ya miundombinu itakayojengwa katika kituo hicho ambapo amesema kazi hiyo itafanyika kwa miezi sita na ujenzi unatarajiwa kuchukua miezi 12 mpaka kukamilika.

Msanifu Majengo Yassini amesema kazi ya ubunifu wa michoro inahusisha hostel, madarasa,kumbi za mihadhara, karakana pamoja na ofisi za wakufunzi na watumishi wa kituo hicho ambapo amesisitiza kuwa miundombinu yote inayobuniwa inawezesha kituo kuchukua wanafunzi 650 kwa wakati mmoja.