April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nchemba aiomba WFP kununua nafaka za wakulima hapa nchini kulisha wakimbizi katika maeneo wanayoyahudumia

Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), kununua shehena ya nafaka kutoka kwa wakulima hapa nchini kwa ajili ya matumizi yake ya kulisha wakimbizi maeneo mbalimbali wanayoyahudumia.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo Bi. Sarah Gibson, ambapo wawili hao wamejadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 6 kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021, Tanzania imezalisha ziada ya chakula kiasi cha tani milioni 17.8 na kwamba ukosefu wa soko la mazao hayo ya kilimo unakwamisha juhudi za wakulima kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Nchemba aliliomba Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kusaidia upatikanaji wa masoko na fedha kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kutakako iwezesha nchi kuzalisha chakula kwa wingi na kuwezesha Tanzania kuwa ghala la chakula.

“Rai ya Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuendelea kushirikiana katika maeneo ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ameyawekea kipaumbele ya kutafuta masoko ya bidhaa za wakulima wetu kwahiyo WFP na maeneo mnayoyahudumia mnaweza kusaidia kupata masoko ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji wao” Alisema Dkt. Nchemba.

Alilipongeza Shirika hilo kwa juhudi zake za kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto na kuliomba kuendelea kusaidia eneo hilo kwa kuleta mawazo yenye ubunifu wa namna ya kukomesha tatizo hilo nchini.

Aidha, Dkt. Nchemba aliliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa kuiwezesha Serikali kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi itakayosaidia kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), Sarah Gibson, alisema kuwa msimu huu, Shirika lake limenunua tani 76,000 za chakula nchini Tanzania kwa gharama ya dola za Marekani milioni 25 na kuzisambaza kwenye maeneo yenye uhitaji.

“Katika kipindi hicho pia tumetumia kiasi cha dola za Marekani milioni 19 kwa ajili ya kuboresha shughuli za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha chakula kinachopelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji hususan maeneo ya wakimbizi” alisema Bi. Gibson

Alidokeza kuwa Shirika lake limepanga kutumia zaidi ya dola za Marekani milioni 336 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia Mwaka 2022 hadi mwaka 2027 ambapo wanatarajia kuwafikia zaidi ya watu milioni moja.

Bi. Sarah Gibson alisema pia kuwa Shirika lake limepanga kurejesha huduma ya chakula mashuleni hapa nchini baada ya kusitisha huduma hiyo miaka michache iliyopita kutokana na umuhimu wa chakula kwa watoto wakiwa shuleni

“Pia tumepanga kuanzisha mpango wa kuwasaidia watu kupata fedha taslimu kwa njia ya kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo miradi ya kilimo, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuwapatia mikopo midogo midogo pamoja na masoko ya uhakika wakulima wadogo wadogo” alisema Bi. Gibson