August 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GF yaahidi kuendelea kuunga mkono maono ya Serikali

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya GF Vehicle Assemblers imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza viwanda vya ndani, kupitia uunganishaji na uzalishaji wa magari na mitambo nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.

Dhamira hiyo imeelezwa Agost 4 mjini Kibaha na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Ezra Mereng, alipokuwa akitoa taarifa kwa
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo aliyefanya ziara katika Kiwanda hicho.

Naibu Waziri huyo alitembelea kiwanda hicho kujionea uwezo wa uzalishaji, uunganishaji wa magari na maendeleo ya teknolojia yanayolenga kuongeza thamani ya bidhaa zinazotengenezwa nchini.

Mereng, amesema kampuni hiyo imejipanga kuendeleza uwekezaji wake katika teknolojia ya kisasa na kuwajengea uwezo watalaamu wa ndani.

“GF inaamini kuwa uwekezaji katika uzalishaji na uunganishaji wa bidhaa nchini Tanzania ni hatua muhimu katika kujenga uchumi shindani, kuongeza ujuzi wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya viwanda,” amesema Mereng.

Kwa upande wake, Denis Londo amepongeza kampuni ya GF kwa hatua hiyo na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo kuu ya kuharakisha maendeleo ya Viwanda nchini.

Londo ameongeza kuwa jitihada hizo zitasaidia kuongeza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania na kupunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa zilizokamilika kutoka nje ya nchi, jambo linaloimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na lile la Eneo la Biashara Serestu la Afrika (AfCFTA).

Pia amesema Serikali inasimamia utaratibu wake wa kudhibiti uingizwaji bidhaa ambazo hazizalishwi ndani ya nchi ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Londo amesema wawekezaji wa viwanda wanatakiwa kuanza kuzalisha bidhaa nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya ndani na ya Viwanda vingine.