May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jaji Feleshi: Tupo pamoja kuelekea mabadiliko ya Sheria ya Habari

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Eliezer Feleshi amesem kuwa ofisi yake ipo pamoja na hatua zinazochukuliwa na wanahabari katika kuyaendea mabadiliko yanayotakiwa.

Jaji Feleshi ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Juni 2022, ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma alipokutana na wadau wa habari.

“Niko na nyinyi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) katika hatua kuelekea mabadiliko ya sheria za habari.

Jaji amependekeza kuwepo na bodi ya wanahabari itakayosimamiwa na wanahabari.

Amesema, chombo hicho ndio kitachokuwa na wajibu wa kusimamia wanahabari na hata kuwashughulikia endapo watakwenda kinyume na maadili ya habari.

“Sina tatizo, naona muwe na ‘regulator’, bodi yenu moja, ili mmoja wenu akienda kinyume na maadili (ya uandishi wa habari), mnamshughulikia nyinyi wenyewe,” amesema Jaji Eliezer Feleshi.

Jaji Feleshi ametoa kauli hiyo baada ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kumweleza kuwa, wanahabari wanapendekwa kuundwa kwa chombo kimoja kitakachosimamia wanahabari badala ya vyombo vinne kama inavyoelekezwa na Sheria ya sasa.

Pia Balile amemweleza Jaji Feleshi kuwa, miongoni mwa mambo yanayotisha wanahabari katika sheria iliyopo sawa, anaweza kufungwa bila hata ya yeye (mwanahabari) kuitwa kusikiliza kesi yake.

Jaji Feleshi amesema, sheria yoyote lazima ipitiwe vizuri na iwe na uhalali lakini pia iwe ya wananchi.