May 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yavuka lengo utoaji chanjo ya polio

Na Judith Ferdinand,Mwanza

KAMPENI ya utoaji chanjo ya polio kwa njia ya matone awamu ya pili kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10, imekamilika Mei 10,2026, huku Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ikifanikiwa kuvuka lengo kwa asilimia 103.

Ambapo halmshauri hiyo ilifanikiwa kuwachanja jumla ya watoto 181,178, huku  lengo likiwa ni kuwafikia  watoto 174,644.

Kampeni hiyo ambayo imefanyika kwa Mikoa saba ikiwemo Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu,Mara,Tabora na Singida  kwa siku nne kuanzia Mei 7 -10,2026,ni jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwakinga watoto na virusi hatari vienezavyo ugonjwa wa polio.

Akizungumza  jana,Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Shamte Almasi amesema, baada ya kutolewa kwa chanjo hiyo  ya polio aina ya noVP2,anaamini kuwa watoto sasa wako salama.

Shamte ametumia fursa hiyo  kutoa wito kwa wazazi kuwa na mwamko wa kuwapatia watoto wao chanjo mbalimbali kama ilivyokua kwenye chanjo hiyo,ili kuweza kuwakinga na maradhi mbalimbali.

Muuguzi na Mratibu wa Chanjo Kituo cha Afya Buzuruga,Damarice Dawson  amesema,muitikio umekua mkubwa kwa wazazi kuwaleta watoto wao  kupata chanjo hiyo,hivyo aliwapongeza kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha kampeni.

Kwa upande wake Furaha Mwita mkazi wa  Kata ya Buzuruga,amesema anafuraha watoto wake  wamepata chanjo  hiyo,hivyo anaamini  watakuwa salama.

Naye Majani Maharage mkazi wa Buzuruga,amesema  ni mara ya kwanza kumpeleka mtoto wake   kupata chanjo ya polio ambayo ni nzuri kwa afya ya watoto huku akiwasisitiza wazazi wengine kushiriki kampeni kama hizo.

“Tumeletewa chanjo bure hakuna gharama yoyote.Chanjo ni nzuri na haina madhara yoyote,”amesema Mwanne Ally mkazi wa  mtaa wa Buzuruga Kusini.