May 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaodai fidia walipwe ndani ya miezi mitatu

Na Judith Ferdinand,Mwanza

UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,umetakiwa ndani ya miezi mitatu kuanzia Mei hadi Julai 2026, kuhakikisha wanawalipa fidia wananchi wote waliopisha maeneo yao kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Agizo hilo amelitoa Mei 12,2026 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata za Sangabuye,Bugogwa na Kayenze uliofanyika mtaa wa Nyafula,wilayani Ilemela mkoani Mwanza kwa ajili ya kusikiliiza na kutatua kero mbalimbali.

Ambapo aliwapa pole na kuwapongeza wananchi hao wanaodai fidia tangu mwaka 2022 kwa moyo wa uvumilivu waliouonesha kwa kipindi chote.

“Madai yenu yote yatalipwa.Nakuaelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,kwa kipindi hicho cha miezi mitatu,wananchi wote wanaodai fidia wawe wamelipwa,na kuanzia sasa hakuna kuchukua eneo lolote kabla ya kulipa fidia,”amesema Mtanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Amiri Mkalipa,ameahidi kuwa maelekezo yote aliyotoa Mkuu huyo wa Mkoa,watayatekeleza kama alivyoagiza na anaamini kuwa changamoto zilizotolewa na wananchi zitaendelea kutatuliwa na kumalizwa kabisa.

Naye mmoja wa wananchi kutoka mtaa wa Nyafula Kata ya Sangabuye Agnes Kakila, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya mkutano,kuwasilikiza na kutatua kero zao zilizokuwa zinawasumbua kwa muda mrefu ikiwemo maji, umeme na barabara.

Ambapo kupitia yeye zimeweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu huku wananchi wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kufanya kazi, kulinda amani na kuiletea nchi maendeleo.