

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeadhimisha siku ya Afya ya Mimea Duniani huku serikali ikisema itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa ili kuhakikisha taasisi hiyo inatoa huduma bora zaidi katika kulinda afya ya mimea, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumza jijini Dodoma katika maadhimisho hayo ambayo hufanyika Mei 12 ya kila mwaka Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Daniel Godfrey Chongolo, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Duniani yaliyoandaliwa na TPHPA.
Silinde amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa afya ya mimea katika kuongeza tija ya mazao, kuzalisha ajira, kuimarisha usalama wa chakula na lishe pamoja na kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo.
Amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali inalenga kuongeza ushirikiano wa TPHPA katika kusimamia afya ya mimea, wanyama, binadamu na mazingira ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
“Katika kukabiliana na changamoto za afya ya mimea, tunahitaji ushirikiano na hatua za pamoja,ikumbukwe hakuna nchi, taasisi au sekta binafsi inayoweza kukabiliana pekee na changamoto za visumbufu vya mimea na mazao,” amesema Silinde.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema mamlaka hiyo imeendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha usalama na utoshelevu wa chakula nchini.
Amesema mwaka 2024/2025 Tanzania ilikuwa na utoshelevu wa chakula wa asilimia 130 ambapo uzalishaji wa chakula ulifikia tani 23,783,128 kutokana na juhudi mbalimbali za kudhibiti visumbufu vya mazao.
Profesa Ndunguru amesema TPHPA imefanikiwa kudhibiti baa la panya katika mikoa 19, wilaya 68, kata 638 na vijiji 1,669 ambapo zaidi ya ekari 408,109 za mazao ziliokolewa huku wakulima 66,511 wakinufaika.
Aidha, amesema mamlaka hiyo ilidhibiti zaidi ya ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea milioni 231 waliovamia mashamba ya nafaka katika mikoa mbalimbali nchini na kuokoa takribani tani 1,611,000 za mazao.
Katika mapambano dhidi ya viwavijeshi, amesema TPHPA ilifanya udhibiti katika hekta 219,411 na kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya mahindi na mtama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mashamba ya vijana wa BBT mkoani Dodoma.
Pia amesema mamlaka hiyo ilifanya utambuzi na udhibiti wa nzige wa miti waliovamia ekari 1,340 katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma pamoja na kudhibiti nzige wekundu zaidi ya milioni 38 katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa kulinda afya ya mlaji na mazingira, Profesa Ndunguru amesema TPHPA imeanzisha mfumo wa kufuatilia masalia ya viuatilifu kwenye mazao ya chakula ambapo sampuli 758 za matunda na mboga zilichukuliwa katika mikoa mbalimbali na kubainika kuwa viwango vya masalia vilikuwa ndani ya kiwango kinachokubalika kitaifa na kimataifa.
Amesema mamlaka hiyo pia imeondoa sokoni viuatilifu 130 hatarishi baada ya kufanya uchambuzi wa viambata hatarishi vya viuatilifu nchini.
Katika hatua nyingine, amesema TPHPA imeendelea kufungua masoko ya mazao nje ya nchi kwa kuwezesha kukamilika kwa nyaraka za kufungua masoko katika mataifa 15 kwa mazao mbalimbali ikiwemo parachichi, ndizi, karafuu, vanila, pilipili manga na maua.
Ameongeza kuwa China imeridhia makampuni 16 ya Tanzania kusafirisha parachichi nchini humo baada ya kukidhi viwango vya kimataifa, huku zaidi ya makampuni 410 yakisajiliwa kuuza mazao mbalimbali katika soko la China.
Profesa Ndunguru amesema TPHPA pia imeimarisha miundombinu kwa kununua mashine tano za kisasa za maabara zenye thamani ya Sh bilioni 2.8 pamoja na ndege nyuki 21 za kisasa kwa ajili ya udhibiti wa visumbufu vya mimea.
Aidha, amesema mamlaka hiyo imenunua ndege maalumu ya kunyunyizia viuatilifu yenye uwezo wa kunyunyizia zaidi ya ekari 2,400 kwa wakati mmoja.
Katika kuhifadhi bayoanuai ya mimea, amesema TPHPA imekusanya na kuhifadhi maelfu ya sampuli za mimea pamoja na kugundua aina mpya 12 za mimea zilizotambuliwa kisayansi nchini.

More Stories
Ded Yegella amshukuru Rais Samia kwa ajira 259
Mkakati ondoshaji ongezeko la shehena yatajwa
Wizara,TPSF kuongeza ushiriki kongamano la kiswahili