Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,umetakiwa kujikita katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye kuleta tija kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa Juni 29,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmshauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kupokea na kuzijadili taarifa za ukaguzi wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2024/2025.

“Tutakapokuja mwakani mtuambie ni miradi gani mikubwa mmetekeleza kutokana na mapato ya ndani.Halmashauri haitasifika kwa kujenga matundu ya vyoo wala ujenzi wa vyumba vya madarasa,”amesema Mtanda.
Hata hivyo Mtanda,ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kuendelea kupata hati inayoridhisha kwa miaka minne mfululizo.
Ambapo amesema kuwa Ilemela ni miongoni mwa halmashauri mkoani Mwanza inayofanya vizuri katika suala la ukusanyaji wa mapato kwa mujibu wa takwimu kwani mapato yamekuwa yakipanda mwaka hadi mwaka na hivyo kuitaka kutumia mapato hayo kwa utekelezaji wa miradi mikubwa.
Sanjari na hayo amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mkalipa,kuunda kikosi kazi kitakachohusisha vyombo mbalimbali kwa ajili ya kufuatilia madeni ya mikopo hiyo ya asilimia 10,huku akisistiza kuwa fedha za mikopo sio za sadaka ni fedha za umma ni lazima zirudi ili kuwezesha wengine kukopa. Hivyo wale wanaodaiwa na hawajarejesha watafutwe na wakamatwe.
Aidha amewataka wananchi wa Wilaya ya Ilemela kuimarisha amani na utulivu kwa uvumilivu,moyo wa kizalendo na ushirikiano katika kuijenga nchi na Ilemela,ambapo alisisitiza kuwa gharama ya ujenzi wa amani ni kubwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amemtaka, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha hoja hazijirudii ikiwa ni pamoja na kufunga hoja za miaka ya nyuma.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, baada ya CAG kukagua hesabu za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela matokeo ya ukaguzi huo ni kwamba halmashauri hiyo ilipata hati safi.

More Stories
Serikali yambana mkandarasi kituo cha umeme Hale
Polisi wachunguza jeneza lililotelekezwa soko la Kabila
Mbaroni kwa tuhuma za ubakaji,uporaji