
Na Israel Mwaisaka, Sumbawanga
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha programu ya mafunzo ya uanagenzi kama mkakati wa kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kazi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiri wengine, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.), amesema hayo Julai 18, 2026 alipokagua utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Kampasi ya Rukwa, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mhe. Sangu alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewawezesha vijana 5,746 kupata mafunzo ya uanagenzi katika vyuo 46 vilivyopo katika mikoa 25 nchini. Alisema Serikali imewagharamia ada za mafunzo, bima ya afya kwa kipindi chote cha mafunzo pamoja na fedha za kujikimu wanapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo.
Alieleza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kujitegemea kiuchumi. Aidha, alibainisha kuwa Serikali itaendelea kupanua fursa za ajira kwa wahitimu wa programu hiyo.
Mhe. Sangu alisema wahitimu wa programu ya uanagenzi mwaka 2026 watapatiwa vifaa vya kuanzia kazi (start-up tools) ili kuwawezesha kujiajiri na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Aidha, alisema Serikali imejipanga kuwaunganisha wahitimu hao na taasisi mbalimbali ikiwemo PPRA kwa ajili ya usajili katika mfumo wa ununuzi wa umma pamoja na taasisi za kifedha zikiwemo benki ili kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Alana Nchimbi, alisema Mkoa wa Rukwa una vyuo viwili vinavyotekeleza programu ya uanagenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo MUST Kampasi ya Rukwa, ambacho kimepokea wanagenzi 154, na kwamba programu hiyo programu hiyo inaendelea kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

More Stories
Sangu atoa onyo matumizi mabaya fedha za miradi
UNDP yanoa watengeneza maudhui Songwe
Watendaji Ubungo wapongeza ubunifu ununuzi wa mitambo