
Na Israel Mwaisaka, Sumbawanga
Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amewataka watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kusimamia kwa uadilifu fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ilete tija na kuwanufaisha wananchi.
Sangu ametoa kauli hiyo jana (20 Julai 2026) wakati akikagua eneo litakalojengwa Shule mpya ya Sekondari Uzia katika Kijiji cha Usangwa, Kata ya Muze, ambapo alisema usimamizi madhubuti wa fedha za umma ni msingi wa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo akisisitiza kuwa fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa bila kuwepo ubadhirifu au matumizi yasiyoidhinishwa.
“Ninawasihi sana viongozi na watendaji wa halmashauri msimamie fedha hizi kwa uadilifu. Tunataka ifikapo Januari 2027 shule hii iwe imekamilika na ipokee wanafunzi wa kidato cha kwanza,” alisema Sangu.
Katika mwendelezo wa ziara yake Sangu alifika Kata ya Mtowisa ambako alikagua jengo la darasa na ofisi ya walimu zilizoezuliwa na upepo mkali mwezi Machi mwaka huu, hali iliyosababisha usumbufu kwa wanafunzi na walimu. Akiwa eneo hilo alikabidhi mabati 126 yenye thamani ya Sh. milioni 3.1 ili kusaidia ukarabati wa majengo hayo.
Mbunge huyo pia alisema Hospitali ya Wilaya iliyopo Mtowisa inapaswa kuanza kutoa huduma kikamilifu kwa kuwa miundombinu yake imefikia hatua nzuri, huku akiahidi kushughulikia changamoto zilizobaki ili wananchi wapate huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
Diwani wa Kata ya Muze, Mhe. Kalolo Ntilla alisema ujenzi wa Shule ya Sekondari Uzia umetokana na juhudi za Mbunge Sangu za kusukuma maendeleo ya sekta ya elimu akieleza kuwa mradi huo utaondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya elimu ya sekondari.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mtowisa, Mhe. Paulina Kisiwa alimuomba Mbunge huyo kuendelea kuiomba Serikali kukarabati barabara za kata hiyo ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka vijijini kwenda kwenye masoko na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.
Waziri Sangu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika Jimbo la Kwela kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao, kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

More Stories
Mpango wa Serikali wa uanangezi wawanufaisha halmashauri Sumbawanga
UNDP yanoa watengeneza maudhui Songwe
Watendaji Ubungo wapongeza ubunifu ununuzi wa mitambo