Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
PASCHAL Sangisangi(27),mkazi wa Kijiji cha Mwabului wilayani Sengerema mkoani Mwanza,anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya ubakaji,uporaji na kujeruhi.
Ambapo imedaiwa kuripotiwa taarifa katika Kituo cha Polisi Sengerema kuhusu kuwepo kwa kijana ambaye amekuwa akiwarubuni mabinti kwa kuwapigia simu,kisha kukutana nao mafichoni na kuwaingilia kimwili bila
ridhaa yao na baadaye kuwapora mali walizokuwa nazo kama simu na fedha
kisha kutoweka.
Akizungumza Juni 29,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa,amesema Juni 6, mwaka huu,binti mwenye umri wa miaka 20, mwanafunzi na mkazi wa Migombani, Kata ya Nyampulukano, wilayani Sengerema(jina limehifadhiwa), alipigiwa simu na mtuhumiwa na kumtongoza huku akimhadaa kuwa angempatia zawadi.
DCP.Mutafungwa amedai kuwa baada ya kupigiwa simu na kuelezea maneno hayo binti huyo alikubali kukutana na kijana huyo, ndipo alipomwingilia kimwili kwa nguvu, kisha kumpora simu yake aina ya Samsung A42 5G yenye thamani ya sh.200,000.Kabla ya kutoweka alimjeruhi kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu ya paji la uso na kumsababishia madhara mwilini.
Pia Juni 10, 2026, majira ya saa 1.00 usiku,eneo la Soweto Mission wilayani Sengerema,binti mwingine mwenye umri wa miaka 17(jina limehifadhiwa), mwanafunzi na mkazi wa eneo hilo, alijeruhiwa na mtuhumiwa huyo kwa kukatwa kwenye paji la uso kwa kutumia kitu chenye ncha kali, jambo lililosababisha kupata madhara mwilini.
“Matukio hayo yaliripotiwa katika Kituo cha Polisi Sengerema na uchunguzi
kuanza mara moja.Ilipofika Juni 20,2026, katika maeneo ya shule ya
Msingi Igogo wilayani Sengerema, mtuhumiwa alitiwa mbaroni na Jeshi la
Polisi akiwa na simu yake ya mkononi aliyokuwa akiitumia kuwapigia mabinti
na kuwahadaa, kisha kuwafanyia matukio hayo ya ubakaji, uporaji na kujeruhi,”amesema DCP.Mutafungwa.
Hata hivyo amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na jeshi hilo kuhusiana tuhuma za matukio hayo.Huku akitoa wito kwa mabinti na watu wengine waliofanyiwa matukio kama hayo wasione aibu kufika katika vituo vya polisi na kutoa taarifa kuhusu
mtuhumiwa huyo au watuhumiwa wengine kwani katika vituo hivyo kuna madawati ya ukatili wa kijinsia na watoto.

More Stories
Serikali yambana mkandarasi kituo cha umeme Hale
Polisi wachunguza jeneza lililotelekezwa soko la Kabila
Ilemela yatakiwa kutekeleza miradi mikubwa