June 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi wachunguza jeneza lililotelekezwa soko la Kabila

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio la kuonekana kwa jeneza dogo likiwa limetelekezwa katika uwanja wa soko la mnada la Kabila uliopo Kata ya Kabila wilayani Magu mkoani Mwanza.

Akizungumza Juni 29,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa,amesema Juni 29,2026, majira ya saa 11.00 alfajiri,jeshi hilo lilipokea taarifa juu ya tukio hilo kutoka kwa wananchi na wakazi wa  maeneo hayo.

Baada ya kupokea taarifa hiyo mara moja jeshi hilo lilifika eneo la tukio na kulifanyia uchunguzi jeneza hilo lilikuwa na rangi ya zambarau na msalaba wenye rangi nyeupe ambapo ndani yake vilikutwa vipande vya nyama,kichwa na miguu ya kondoo, pamoja na dawa za kienyeji.

DCP.Mutafungwa alisema,uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea huku akiwaomba wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu na wasiwe na imani potofu za kishirikina zinazoweza kusababisha taharuki katika jamii au kuwashambulia kwa namna yoyote ile watu wengine kwa tuhuma za ushirikina.