Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
SERIKALI imemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ukarabati wa kituo cha kufua umeme cha Hale mkoani Tanga kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliobaki wa mkataba bila kuomba nyongeza nyingine.
Serikali imesema kukamilika kwa mradi huo kutarejesha uzalishaji wa megawati 21 za umeme, hatua itakayoongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kaskazini ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.

Akizungumza Juni 29,2026 wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kituo cha Hale kilipoanza kufanya kazi baada ya uhuru kilikuwa kinazalisha megawati 21, kiwango kilichokuwa kinatosheleza mahitaji ya Taifa kwa wakati huo ambapo matumizi ya umeme yalikuwa takribani megawati 36.
Amesema kadri miaka ilivyopita, mitambo ya kituo hicho, ambayo sasa ina zaidi ya miaka 60, ilichakaa na kusababisha uwezo wa uzalishaji kushuka kutoka megawati 21 hadi megawati 6 pekee.
“Kutokana na uchakavu huo, Serikali ya kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA),ilitoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki.Ambapo Serikali ya Tanzania imechangia asilimia 40 ya gharama za mradi huku Serikali ya Sweden kupitia SIDA ikichangia asilimia 60, na kufanya jumla ya gharama kufikia takribani sh.bilioni 64,”amesema Ndejembi.
Ameeleza kuwa fedha hizo zimetumika kufunga mitambo mipya ya kisasa yenye lengo la kurejesha uwezo wa kituo hicho kuzalisha megawati 21 kama ilivyokuwa awali.Huku akisisitiza kuwa Serikali haijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, kwani ulitakiwa kuwa umekamilika miezi 10 iliyopita.
“Mradi huu uko nyuma ya ratiba.Leo tumemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kabla ya Julai 31 mwaka huu, ambao ndiyo mwisho wa mkataba wake. Hatutatoa nyongeza nyingine kwa sababu tayari aliongezewa muda Machi ili aweze kukamilisha kazi,”amesema Ndejembi.
Amebainisha kuwa jambo la kutia matumaini ni kwamba asilimia 98 ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi tayari vimewasili eneo la mradi na mafundi wanaendelea na kazi, hivyo matarajio ni kuona uzalishaji wa megawati 21 unaanza mara baada ya mradi kukamilika.
Kwa mujibu wa Ndejembi, kuongezeka kwa umeme huo kutasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati katika mikoa ya Kaskazini, hususani Mkoa wa Tanga ambao kwa sasa unatumia takribani megawati 130 kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi na viwanda.
Amesema pamoja na kufunga mitambo mipya ya kuzalisha umeme, mradi huo unahusisha pia uwekaji wa transfoma kubwa yenye uwezo wa kupokea na kusambaza umeme mwingi zaidi pamoja na kubadilisha nyaya za zamani zilizowekwa mwaka 1964 ambazo uwezo wake wa kusafirisha umeme ulikuwa mdogo.
“Hatua hizi zitaimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa mikoa ya Kaskazini. Umeme si anasa, ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya sekta za afya, elimu, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji,”amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme wa TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya,amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo ya Serikali na itaendelea kumsimamia mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi na endapo kutakuwa na ukiukwaji wa masharti ya mkataba, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa vifungu vya mkataba.
Hata hivyo mradi huo unahusisha ujenzi wa mitambo mipya pamoja na kituo cha kupooza umeme. Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 83, huku Serikali ikitarajia mradi huo kukamilika ifikapo Julai 31 mwaka huu.


More Stories
Polisi wachunguza jeneza lililotelekezwa soko la Kabila
Mbaroni kwa tuhuma za ubakaji,uporaji
Ilemela yatakiwa kutekeleza miradi mikubwa