April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGP Sirro kuendelea kuongoza EAPCCO

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira, Online

SHIRIKISHO la Wakuu wa Polisi Mashariki Mwa Afrika (EAPCCO) wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kuendelea kuwa mwenyekiti wa Shirikisho hilo kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.

Uamuzi huo umetolewa leo na nchi 14 wanachama wa Shirikisho hilo kupitia mkutano wake mkuu wa 22 wa mwaka uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference) ambapo wakuu hao walisema kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa Corona kumesababisha mambo mengi ya shirikisho hilo kutokamilika kwa wakati.

Hata hivyo, IGP Sirro amesema hadi sasa Shirikisho hilo limepata mafanikio makubwa huku akieleza kuwa katika kipindi cha 2021 wamejipanga kutekeleza yale ambayo hayakuweza kufikiwa na watahakikisha kuwa nchi wanachama wataweza kubadilishana uzoefu na kufanya mafunzo ya pamoja ya mbinu za medani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, IGP Sirro amesema kuwa, kutokana na ushirikiano wa Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika kumewezesha kudhibiti uhalifu wa kupanga na unaovuka mipaka, usafirishaji wa nyara za serikali sambamba na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji binadamu na dawa za kulevya, alisema IGP Sirro.

Aidha, IGP Sirro anaendelea tena kuongoza shirikisho hilo kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja tangu pale alipochaguliwa katika mkutano mkuu wa 21 wa mwaka uliofanyika mwezi Septemba mwaka jana jijini Arusha.