May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yaweka mikakati thabiti kumtua mama kuni

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI   imejipanga kuhakikisha  ifikapo mwaka 2033 asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wawe wanatumia  nishati safi ya kupikia ili kuondomana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo kwa kiasi kikubwa husababisha uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji moti hovyo

Hayo yamesemwa na  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa  huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt.James Andilile wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kongamano la wanawake la Nishati safi ya kupikia ambalo lilienda sambamba na ugawaji wa nishati safi ya kupikia kwa akina wajasiriamali.

Amesema   kama Taifa  bado matumizi ya  nishati chafu ya kupikia kwa maana ya matumizi ya kuni na mkaa bado ni makubwa na kwamba jitihada za kubadilisha matumizi ya nishati hiyo bado zinahitajika.

Amesema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa EWURA inajielekeza katika maeneo mawili ambayo ni pamoja na  kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi kwa kuhakikisha wanatoa  vibali kwa wawekezaji kwa wakati sambamba na kusimamia  suala la upatikanaji  na usambazaji wa nishati katika maeneo ya vijijini .

Kwa mujibu wa  takwimu  za mwaka 2015 zinaonesha kwamba takribani asilimia 80 ya nishati inayotumiwa si safi, na nishati hiyo inayotumika inatokana na mkaa  pamoja na kuni.

“Lakini katika juhudi za Serikali  za  kukabiliana na changamoto zinazotokana na  kutotumia nishati safi ikiwemo madhara ya afya yatokanayo na moshi pia ikiwemo  suala la madhara katika mazingira na muda pia wa kupika  hususani kwa kina mama ambao wanatumia muda mwingi wa kwenda kusaka kuni imejidhatiti kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati safi ya kupikia” amesema Dkt.Andilile na kuongeza kuwa

“Kama Serikali ilivyofanikiwa kumtua mama ndoo kichwani na  sisi EWURA  tutaenda kumtua mama kuni kichwani”Amesema Dkt.Andilile