May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA ilivyojipanga upatikanaji rahisi wa gesi

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MKURUGENZI wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage amesema,Wakala huo  umejipanga kuhakikisha  wananchi hususan waishio vijijini wanapata nishati safi ya kupikia na kwa bei rahisi.

 Akizungumza jijini Dodoma na waandishi wa habari katika maonesho ya Kongamano la Wanawake la Nishati Mbadala Mhandisi  Mwijage amesema changamoto iliyopo kwa sasa  ni kwamba, nishati inaweza kupelekwa vijijini lakini endapo ikakosekana nishati inayoendana  kwenye maeneo hayo wananchi watarudi kwenye  matumizi yao ya kila siku  ya kuni.

Kwa mujibu wa mhandisi Mwijage,bado ipo kazi kubwa  ya kuhakikisha kwamba nishati zote za kupikia  zinazotangazwa  zinapelekwa mpaka  kwenye  maeneo ya vijijini  na pia iwajengee wao nidhamu ya kuweza kutoa fedha zao mfukoni na kuweza kununua aina za nishati wanazozitaka,

“Sisi kama wakala tunazo programu mbalimbali  na ya kwanza ambayo imeanza  ni programu ya kusambaza gesi asilia  katika mkoa wa Lindi na Pwani na mtandao huu utasambazwa karibu kwa wananchi 980 kwa kuanzia ambapo  gharama yake ni shilingi bilioni 6.8″alisema Mhandisi Mwijage

Amesema  mradi utakaofuatia utakuwa na gharama ya shilingi  Bilion 13.5 na mradi huo utawanufaisha wananchi wa mkoa wa mtwara na Pwani  wapatao 1400.

Ametoa wiyo kwa wananchi kwenye maeneo wanayopitiwa na bomba kuu la gesi asilia wakae tayari na wawe tayari kupokea mradi wa serikali  na kutoa ushirikiano mkubwa hususani kwenye masuala ya miundombinu ya gesi itakayopita chini kwenye mashamba yao kwa urahisi.

Aidha ameutaja  mradi mwingine walionao ni wa kusambaza mitungi ya gesi vijijini ambapo hadi sasa mitungi  74,600 imeshasambazwa na mradi bado unaendelea.