April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC, Lijualikali apiga marufuku shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji



‎Na Israel Mwaisaka,Rukwa

‎Mkuu wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Peter Lijualikali amepiga marufuku  uendeshaji shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kando ya Mito, Mabwawa na vyanzo vya maji na kuelekeza hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mtu au watu ambao watabainika kungilia vyanzo hivyo.

‎Lijualikali ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uwekaji vigingi vya mipaka (beacon) kwenye vyanzo vya maji katika kijiji cha Kantawa kata ya Kipande wilayani humo na kusema lengo la serikali ni kulinda na kutunza vyanzo vya maji ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikiharibiwa kwa makusudi kutokana na uwepo wa shughuli za kibindamu kando ya vyanzo vya maji.

‎Aidha ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa serikali za vijiji na kata wilayani humo, kudhibiti uharibifu wa miundombinu ya maji ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji.

‎Afisa mazingira kutoka Bodi ya Maji Bonde la ziwa Rukwa Musaba Joseph, amesema zoezi hilo linaendeshwa kwenye vyanzo vitatu vya maji kwa kuweka vigingi mia sita (600) ikiwa ni pamoja na kupanda miti elfu tatu (3000) ambayo ni rafiki kwa mazingira kuzunguka maeneo husika.

‎Hata hivyo imeelezwa kuwa uwepo wa vigingi vya mipaka kando ya mito, mabwawa na vyanzo vya maji vitasaidia kuongeza hali ya upoatikanaji wa maji wilayani humo.