April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Korogwe ataka misitu itunzwe kuepuka maafa

“Meneja wa TFS Wilaya ya Korogwe, Mponie Mwaluseke, akipanda mti.”

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amewataka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakishirikiana na wadau wengine kuhakikisha wanapanda miti ili kurudisha uoto wa asili na kuweza kuzuia majanga ya mafuriko na ukame.

Ameyasema hayo leo Machi 24, 2026 kwenye Siku ya Misitu Duniani ambapo alishiriki kwenye zoezi la upandaji miti Msitu wa Lukoka unaozungukwa na vijiji vya Vugiri na Magundi vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na mitaa ya Kwasemangube, Makwei, na Magunga iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe.

Mwakilema amesema miti inayopandwa anataka itunzwe na kukua ili iweze kuungana na ile mingine iliyopo kwenye misitu mbalimbali kwenye halmashauri zote mbili za Korogwe DC na Korogwe TC ili kuweza kuzuia majanga, kwani athari za wananchi kuathirika kutokana na ukataji wa miti ni za wazi, kwani hata usiku wa kuamkia juzi (Machi 23) Soko la Manundu mjini Korogwe lilikumbwa na mafuriko usiku wa manane baada ya Mto Mbeza kufurika, na kufanya maji kujaa kwenye soko hilo.

“Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Baraka Juma akisoma taarifa.”

“Kamati ya Mazingira, viongozi wa chama (CCM Kata) na Serikali, tufanye kazi halisi ya hili zoezi tulilojia hapa la kupanda miti. Lakini nataka kutoa rai, zoezi hili liendelee na maeneo mengine katika halmashauri hizi mbili kwa wananchi kupanda miti ya asili. Ninyi nyote ni mashahidi kwa kile kilichotokea jana. Nilikuwa nakagua maeneo ya watu na Soko la Manundu, nimeona namna watu na wafanyabiashara walivyoathirika na mvua, ambapo hawakulala akiwemo diwani wao (Kata ya Manundu, Rajab Mzige).

“Athari hizo zilitokana na mvua zilizonyesha huku milimani, na kwa sababu milima imekuwa kipara kwa watu kukata miti hovyo, kuchoma mkaa, mabonde yote yamelimwa, Mto Mbeza umekufa, hivyo kufanya maji kutawanyika na kuingia kwenye makazi ya watu na sokoni. Watu wamepata athari kubwa sana. Tumeunda timu ya kuweza kuchunguza athari zilizopatikana ikiwemo za mali. Haya yote mnasema ni Mabadiliko ya Tabianchi, lakini sio kweli, haya ni mabadiliko ya tabia za wanadamu” amesema Mwakilema.

Mwakilema amesema nchi ilikuwa njema ikiwa imesheheni misitu ya asili yenye milima na mabonde yenye rutuba, lakini kutokana na shughuli za binadamu, uoto wa asili umeondoka, sasa ni wakati wa halmashauri kushirikiana na wadau na wananchi kurudisha uoto huo ili kuepuka madhara kama yale ya Soko la Manundu.

“Mtumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Korogwe Saidi Jitihadi akipanda mti.”

“Hivyo niwapongeze Halmashauri ya Wilaya na Wakala wa Misitu (TFS) kwa kuandaa zoezi hili, na ninaomba liwe endelevu kwa kuhakikisha miti ya asili inatunzwa na haikatwi hovyo kwa ajili.ya kuchoma mkaa wala kuungua moto. Na tunatakiwa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutumia nishati safi ya kupikia” alisema Mwakilema.

“Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Baraka Juma akipanda mti.”

Akisoma taarifa, Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Baraka Juma amesema hiyo ni mara ya pili kusherehekea Siku ya Misitu Duniani kwa kupanda miti, kwani mwaka 2024/2025 walifanya hivyo Msitu wa Mfundia na Mazimunyu kwa kupanda miti 36,000 ikiwa ni sawa na asilimia 60 kwa lengo la kupanda miti 60,000.

“Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema akizungumza akiwa kwenye zoezi la upandaji miti.”

“Msimu huu wa 2025/2026 tuna lengo la kupanda miti 10,000 Msitu wa Lukoka wenye ukubwa wa hekta 236 kwa kushirikiana na wadau wa Forest Focus, ambapo miti 5,000 itatoka kwenye vitalu vya halmashauri na mingine 5,000 itatoka vitalu vya Forest Focus.

“Hivyo, leo unazindua zoezi hili kwa kupanda miti 100 kutoka vitalu vya halmashauri kwa kushirikiana na TFS ambao wameshasambaza miti 6,300 maeneo mbalimbali Korogwe DC na Korogwe TC kwenye shule, vyuo ikiwemo cha VETA, taasisi za kidini na watu binafsi” amesema Juma.

Juma amesema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe imebarikiwa kuwa na misitu ya vijiji na halmashauri 11 yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 4,000, misitu inayomilikiwa na TFS tisa yenye ukubwa wa wastani wa zaidi ya hekta 18,000 (ikiwemo Korogwe TC), na watu binafsi hekta 500.

Amesema halmashauri hiyo kwa kushirikiana na World Wildlife Fund (WWF), wamefanya tathmini ya ufanisi wa usimamizi wa misitu, ambapo Msitu wa Mfundia umepata asilimia 63.89 (nzuri), na Mazimunyu asilimia 52 (wastani). Na zoezi hilo ni endelevu kwa misitu mingine kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uhifadhi.

“Mwakilema akipanda mti Msitu wa Lukoka.”

“Tumekamilisha uwekaji wa Plot 70 kwa ajili ya Upimaji wa Carbon katika Msitu wa Mfundia. Hii ni hatua kubwa kuelekea biashara ya Carbon itakayoleta manufaa ya kiuchumi kwa vijiji vyetu vinavyozungukwa na misitu. Na tumepata ushirikiano na jamii kwa kufanya kazi na vijiji vyote vinavyozingukwa na misitu” amesema Juma.

Juma amesema moja ya changamoto ni uvamizi ndani ya misitu, uwepo wa mashamba na makazi ndani ya hifadhi hususani Kijiji cha Mkwajuni, ambapo Plot tatu za Carbon zimevamiwa. Mabadiliko ya Tabianchi, ukame unaoathiri uoto wa asili na juhudi za upandaji miti. Lakini pia uhaba wa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya doria na utunzaji wa takwimu.

“Diwani wa Kata ya Magunga, Daud Ngulizi, akipanda mti.”