May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CWT yakunwa na utendaji wa Rais Samia

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online Igunga.

CHAMA cha Walimu (CWT) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora,kimeeleza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia katika sekta ya elimu nchini unaleta tija na ufanisi.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa CWT Wilaya Igunga Sophia Maziku alipozungumza na TimesMajira Online ofisini kwake mjini Igunga mapema leo,ambapo ameeleza kuwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zinatoa muelekeo chanya wa ukuaji wa sekta ya elimu nchini.

“Kwa niaba ya walimu wilayani Igunga tunampongeza sana Rais Samia kwa jinsi ambavyo serikali yake inavyotatua changamoto za elimu kwa kujenga madarasa,nyumba za walimu sambamba na kuboresha maslahi ya walimu kote nchini,”amesema Maziku.

Ameongeza kusema kuwa,hatua ya serikali kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu, kupandisha madaraja pamoja na kuanza kuongeza nyongeza ya mishahara kila mwaka imeongeza hali na mori ya walimu kufanya kazi.

“Ahadi ya Rais katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi,kuwa wafanyakazi kote nchini mambo yao yatakuwa moto kuanzia bajeti ya 2023/2024 itakayo anza kutekelezwa mwezi Julai mwaka huu imewatoa tabasamu wafanyakazi wote hususani walimu wa wilaya ya Igunga,”amesema Maziku.

Katika hatua nyingine CWT wilayani Igunga imeahidi kuwa bega kwa bega na Rais Samia, watamuunga mkono kwa hali na mali ili aweze kumaliza vipindi vyake viwili vya uongozi.

“CWT Igunga hatuto muacha, mpaka 2030, tunamuhakikishia kuwa tupo naye bega kwa bega kumsaidia lolote, sisi ni wafuasi wake pia ni watu wake, tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu afya njema katika majukumu yake ya kila siku,”amesema Maziku.

Kwa upande wao baadhi ya Walimu akiwemo,Katibu CWT Wanawake,mwalimu shule ya msingi Mwenge,Bernadetha Mswazi, amemshukuru Rais Samia kwa kuipatia Wilaya ya Igunga fedha za maendeleo katika sekta ya elimu ambazo zitatatua changamoto zinazo ikabili sekta hiyo wilayani humo.

“Nampongeze Rais Samia kwa kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu, pia katika shule yangu ya msingi Mwenge tunajengewa darasa la mafunzo kazini kwa walimu (Cluster) jambo ambalo litatusaidia kujifunzia na kufundisha, kwani kila siku mambo yanabadirika katika sekta ya elimu,”amesema Mswazi.

Pia amesema,ujenzi wa madarasa utapunguza mrudikano darsani kwani kwa sasa darasa moja lina wanafunzi 70 mpaka 100 jambo ambalo linawafanya wanafunzi kutokuelewa kwa usahihi.

Mwalimu Alphonsina Mashauri, amesema kuwa kuwa ajira za walimu zilizotolewa zitasaidia walimu kuwa na wanafunzi wachache kwani watagawanywa kulinga na vipindi hivyo kuwafanya kufundisha kwa weledi na usahihi.

“Naishukuru serikali kwa kutoa ajira mbalimbali hasa kada ya ualimu ambayo itasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu na kuongeza ufanisi katika ufundishaji,kwani kwa sasa unakuta darasa moja lenye mikondo mitatu hadi minne lenye watoto zaidi ya 300 mpaka 400 kwa darasa moja linafundishwa na mwalimu mmoja,” amesema Mashauri.

Mwalimu shule ya Msingi Mwenge, Mussa Sama na Mwalimu Shija Mwandu, wamesema kuwa ujenzi wa nyumba za walimu utapunguza adha ya kuishi mbali na shule na kufanya walimu kuhudhuria katika vipindi kwa wakati.

Pia ujenzi wa uzio katika shule ya Msingi Igunga utasaidia wanafunzi kutokupata ajali za kugongwa na pikipiki kwani shule ipo karibu sana na barabara.