May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc ubungo afunguka kesi ya mzee Kwembe

Na David John

MKUU wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba amefatilia mgogoro wa Ardhi uliopo kati ya Mzee Kulwa Machunde (72) na watoto wa Marehemu dada yake na kusema kuwa mgorogo huo unaoendelea ni mgogoro wa kifamilia ambao unahitaji hekima na busara katika kuutatua na si kuingiza masuala ya uharakati.

Amesema kuwa mgogoro huo unahitaji busara katika kuzungumzia kutokana na ukweli kwamba eneo ambalo wanagombea ni eneo halali la watoto hao.

Mkuu wa Wilaya huyo ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada kufanya mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua zilizochukuliwa baada ya kuripotiwa kwamba suala hilo limefika katika Ofisi ya mkuu wa Wilaya hiyo ya Ubungo.

Komba amesema licha ya kwamba yeye ni mgeni na mgogoro huo kuukuta lakini watu hao walifika katika Ofisi yake na kutoa malalamiko yao ambapo aliweza kuwasikiliza na kubaini kuwa mgogoro huo ni wa kifamilia hivyo ni vema kukaa kwa pamoja na kumaliza mgogoro huo.

Mkuu wa Wilaya amesema ili mgogoro huo uweze kuisha unahitaji hekima nyingi na akili kutatua ili watu hao wabaki katika misingi yao ya umoja.

” Kimsingi wasamehe kuvunjiwa na kuharibiwa mali zao ili kuendelea kumiliki ardhi yao kwasababu kiuhalisia watoto wanahaki japo kwamba bado sijakutana na watoto na haya ni maelezo ya upande mmoja lakini Kwa maelezo yao ndio yamefanya kutoa ushauri kama Kiongozi wa Wilaya hii,”amesema .

Amefafanua kuwa jambo hilo wakilipeleka kiharakati waathirika ni wao kuliko hao watoto hivyo linahitaji hekima busara na akili na bahati mbaya Mzee Machunde hana nyaraka zozote kutoka Kwa dada yake hivyo watulie wawe wapole kwani anaendelea kushughulikia jambo hilo kwani tayari ameshapata maelekezo kwenye ngazi zote ikiwamo kata hadi mtaa.

Awali Mzee Kulwa Machunde amesema yeye yupo kwenye eneo hilo tangu 1983 akiwa kijana mdogo na kwa nyakati hizo zote amekuwa akilitunza na kulisimamia eneo ambalo alikabidhiwa na marehemu Dada yake na wakati huo alikuwa amemchukua kutoka nyumbani kwao Mkoani Mara.