April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRB: Makandarasi jazeni zabuni kwa kutumia TANePS

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Morogoro

MAKANDARASI nchini wameelezwa kuwa matumizi ya mfumo wa manunuzi ya umma kielekroniki (TANePS) ni ya lazima kwao hivyo wanapaswa kuufahamu vyema na kuutumia kwaajili ya kuwasilisha zabuni zao mapema.

Hayo yamesemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Joseph Tango, wakati wa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo na wajibu wa mkandarasi.

Tango amesema ni muhimu kwa makandarasi kufanya maandalizi ya zabuni mapema na kuziwasilisha kwa njia ya mfumo huo kama ni mradi wa serikali kwani tabia ya kufanya kwa mtindo wa zimamoto hauwezi kuleta matokeo mazuri.

“Kwenu nyinyi ujuzi wa kutumia mfumo huu wa kielektroniki ni lazima kwasababu mwajiri mkubwa wa mkandarasi ni serikali na kwa sasa huwezi kushiriki zabuni ya kazi za serikali bila kupitia mfumo huu,” amesema

“Na mjenge kawaida ya kufanya mapema kwani mfumo huu ni wa kielektroniki na chochote kinaweza kutokea na kukufanya uchelewe kuwasilisha zabuni kwa mfano hitilafu ya umeme mahali ulipo au udhaifu wa mtandao wa intaneti haya yote yatakukwamisha,” alisema

Amesema moja ya majukumu ya CRB ni kuwaendeleza makandarasi hivyo lengo la mafunzo hayo ni kunoa ujuzi wa makandarasi ili kukuza uwezo wao wa kushindana katika soko la ndani na hata nje ya nchi.

“Mwenyekiti wa bodi alieleza umuhimu wa mafunzo haya sasa ni kwa umuhimu huo huo bodi ikaona ni vizuri makandarasi wote wajue matumizi ya TANePS kwa sababu hata kama mkijua kutengeneza zabuni kama hamtajua vizuri mfumo huu mtakwama,” amesema

Amesema kwasababu serikali ndiye mwajiri mkubwa wa makandarasi itakuwa vigumu kwao kukua kwani kukua kwa mkandarasi ni kushiriki katika ujenzi wa miradi mingi ya ujenzi na kwamba CRB imekuwa ikihakikisha inatimiza wajibu wake wa kuwapa mafunzo ya aina mbalimbali.

Amewasisitiza wakatumie ujuzi walioupata bila woga wowote kudai haki zao zinapokiukwa kwasababu katika mikataba ya ujenzi ambao huwa wanasaini mkandarasi na mwajiri kila mmoja anawajibu wake na haki zake.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Joseph Tango akifunga mafunzo ya siku tatu kuhusu wajibu wa makandarasi na namna ya kujaza zabuni kielektroniki yaliyoendeshwa na bodi hiyo mkoani Morogoro kwa siku tatu na kumalizika siku ya Ijumaa .

“Uzoefu unaonyesha baadhi ya makandarasi wa ndani wanaogopa kudai haki zao za kimkataba hata kama wanazifahamu kwa kuhofia kuharibu uhusiano wake na mwajiri. Kwa hili naomba makandarasi mbadilike kwasababu mnafahamu wazi wao huwa wanawaadhibu mnapokiuka mikataba bila kusika,” amesema

Naibu Msajili wa Bodi hiyo, anayeshughulikia Tafiti na Maendeleo, David Jere alisema mafunzo hayo yaliwashirkisha makandarasi kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Dodoma, Tanga, Arusha, Njombe, Pwani, Iringa, Kagera, Kigoma, Lindi, Kilimanjaro na Mwanza.

Amesema mafunzo hayo ya siku tatu kuhusu wajibu wa mkandarasi yalilenga kumwezesha mkandarasi kuweza kuandaa zabuni shindani ikiwemo mambo ya kuzingatia kwenye mchakato mzima wa zabuni, namna ya kutengeneza bei shindani na namna ya kuwasilisha zabuni hiyo kitaalamu.

Mhandisi Jere amesema mafunzo hayo ni muhimu na makandarasi pia wamefundishwa kutumia mfumo wa manunuzi ya umma kielektroniki unaoendeshwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA)