Na Joyce Kasiki,Tanga
MWENYEKITI wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Profesa John Kondoro, amesema taasisi hiyo inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu nchini ili kukuza bunifu zao na kuzifikisha katika soko.
Akizungumza na waandiahi wa habari katika banda la Taasisi hiyo ,Profesa Kondoro amesema COSTECH inashiriki katika maonesho na mashindano ya kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayolenga kuhamasisha ubunifu, huku ikitoa fursa kwa wabunifu kuonesha bidhaa na teknolojia walizozibuni.
Amesema mbali na maonesho ya bunifu, mashindano ya maarifa yanayoandaliwa katika matukio hayo yanasaidia pia kuchochea ubunifu miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla.
“Tunakuwepo ili kuchochea ubunifu mbalimbali, kuwezesha ubunifu huo kukua na kuwasaidia wabunifu,” amesema Profesa Kondoro.
Kwa mujibu wa Profesa Kondoro, COSTECH iko tayari kusaidia wabunifu kifedha na kuwezesha bunifu zao kufikia hatua ya kuingia katika soko, badala ya kubaki katika hatua ya mawazo au majaribio.
Amesema COSTECH inashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu na mafunzo ya ufundi, ikiwamo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), pamoja na taasisi za elimu ya juu kama Chuo cha Taifa cha Usafirishaji na Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na Arusha Technical College.
Profesa Kondoro amewataka wabunifu kutumia fursa zinazotolewa na taasisi hizo ili kuboresha uwezo na ubunifu wao, hatua ambayo itawawezesha kuandaa bidhaa zenye ubora na ushindani katika soko.
Amesema ushirikiano kati ya COSTECH, taasisi za elimu na wadau wengine ni muhimu katika kujenga mfumo utakaowawezesha wabunifu kutoka kwenye wazo, kutengeneza bidhaa na hatimaye kufikia soko.

More Stories
NaPA kuongeza ufanisi ukusanyaji mapato Ilemela
Serikali:Usimamizi madhubuti wapunguza udanganyifu mitihani
Vyama vya Siasa vyatakiwa kuwa Mabalozi wa Bima