August 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ITA Yatumia Maonesho Kuhamasisha Vijana Kusoma Kodi


Na Joyce Kasiki, Tanga


CHUO cha Kodi (ITA) kimetumia Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu jijini Tanga kuwaelimisha vijana kuhusu programu za kodi na forodha zinazotolewa na chuo hicho pamoja na namna ya kujiunga.


Afisa Mkuu wa Uhusiano wa Umma wa ITA, Oliver Njunwa, akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa ushiriki wa chuo hicho katika maonesho hayo umelenga kuwapa wananchi, hususan vijana, uelewa kuhusu mafunzo yanayotolewa na chuo.


Amesema maonesho hayo pia yamekuwa fursa kwa wanafunzi kupata majibu ya maswali mbalimbali kuhusu Chuo cha Kodi, ikiwemo programu zinazotolewa na fursa zinazopatikana baada ya kuhitimu.


Njunwa amesema miongoni mwa programu zinazotolewa na chuo hicho ni Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi, inayolenga kuwajengea wanafunzi maarifa na ujuzi katika taaluma hizo.


“Tunatoa elimu kuhusu programu tunazotoa pamoja na fursa mbalimbali kwa vijana. Pia tunajibu maswali ya wanafunzi wanaotaka kujua zaidi kuhusu Chuo cha Kodi,” amesema.


Amesema matumizi ya teknolojia yamekuwa sehemu muhimu katika mafunzo ya kodi na forodha, hivyo chuo kinaendelea kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia katika mazingira ya kujifunza na kazi.


Njunwa amesema vijana waliofika katika banda la ITA walipata fursa ya kupata ufafanuzi kuhusu programu za chuo na namna ya kujiunga.


Amewahimiza vijana kutumia maonesho hayo kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma za kodi na forodha na fursa za elimu zinazotolewa na chuo.