Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Tanga
SERIKALI imeendelea kuongeza uwekezaji katika elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kujenga uwezo wa Watanzania kutengeneza teknolojia na suluhisho za ndani zitakazopunguza utegemezi wa wataalamu na teknolojia kutoka nje.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema hayo Agosti 18, 2026 jijini Tanga wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026.
Profesa Mkenda amesema Tanzania ina wataalamu wenye uwezo mkubwa, lakini wanahitaji mazingira bora na fursa za kutumia maarifa yao katika kubuni bidhaa na huduma zitakazosaidia kutatua changamoto za wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Amesema utafiti na ubunifu vinapaswa kuelekezwa katika maeneo yenye changamoto kubwa kwa jamii, yakiwemo kilimo, afya, uzalishaji na mazingira, huku teknolojia zinazobuniwa zikizingatia matumizi endelevu ya rasilimali na mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Serikali inatoa ufadhili wa asilimia 100 kwa lengo la kujenga sayansi na teknolojia nchini,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeendelea kujenga shule za sayansi katika mikoa mbalimbali na kutoa ufadhili wa elimu ya juu kwa wanafunzi wenye vipaji, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu katika sayansi na teknolojia.
Pia amesema maboresho ya sera na mitaala ya elimu yanaendelea kufanyika ili kuifanya sekta hiyo kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, pamoja na kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya dunia inayobadilika kwa kasi kiteknolojia.
Profesa Mkenda ameeleza kuwa vijana wanaofanya vizuri katika ubunifu wameanza kupata fursa za kushiriki mashindano ya kimataifa, jambo litakalosaidia kupima uwezo wa Tanzania katika teknolojia na ubunifu dhidi ya mataifa mengine.
Amewataka taasisi za elimu, watafiti, wabunifu, vijana na wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kutumia elimu, ujuzi, sayansi na teknolojia kujenga Tanzania yenye uwezo wa kuzalisha wataalamu, bidhaa na teknolojia zenye ushindani ndani na nje ya nchi.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, Waziri Mkenda pia alikabidhi tuzo kwa watafiti 154 waliobobea katika tafiti zilizochapishwa kwenye majarida ya kimataifa. Washindi hao walitoka katika nyanja za sayansi asilia, afya na sayansi shirikishi, kilimo na wanyama, pamoja na uhandisi na TEHAMA, huku wakipatiwa vyeti na zawadi za fedha zenye jumla ya Sh milioni 50.
Katika hatua nyingine, Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR), Maryciana Mhagama, amesema Diplomasia ya Uchumi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalenga kuimarisha nafasi ya nchi kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa, hususan maeneo huru ya biashara barani Afrika.
Mhagama ameyasema hayo katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga, ambako CFR ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
“Pamoja na mambo mengine, Uhusiano wa Kimataifa umeweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Uwekezaji, ukuaji wa Biashara, Mikutano, Utamaduni na Utalii. Kwa kuzingatia fursa zilizopo, Tanzania inaendeleza Diplomasia ya Uchumi katika Uhusiano wa Uwili, Kikanda na Kimataifa,” amesema Mhagama.
Akizungumzia mafunzo yanayotolewa na Kituo hicho, amesema kinaendelea kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa mahiri na wenye weledi kitaaluma, wazalendo na raia wema wenye utayari wa kutoa mchango kwa Taifa.
Amesema Kituo kinatoa mafunzo na kozi mbalimbali katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Kimkakati na Diplomasia ya Uchumi.
Mhagama amesema Kituo kimeandaa mafunzo kuhusu Diplomasia, Itifaki na Ustaarabu, “Diplomacy, Protocol and Etiquette”, yatakayofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, CFR, Dar es Salaam, akiwataka wadau kutoka taasisi za umma na sekta binafsi kutumia fursa hiyo.
.

More Stories
NaPA kuongeza ufanisi ukusanyaji mapato Ilemela
Serikali:Usimamizi madhubuti wapunguza udanganyifu mitihani
Vyama vya Siasa vyatakiwa kuwa Mabalozi wa Bima