April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo:Neema imewafikia wakulima wa korosho mtwara

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo amewahakikishia wakulima wa zao la korosho kutokatwa fedha za pembejeo sababu tayari serikali imetoa Bilioni 60 kwaajili ya pembejeo hizo ikiwemo viwatilifu.

Kauli hiyo ameitoa jana mkoani Mtwara katika kijiji Chigugu wilayani masasi,ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa katika Mkoa huo,alisema
miaka ya nyuma serikali ilikuwa ikitoa bilioni 50 kila msimu ambapo wakulima ukatwa fedha pindi wanapoenda kuuza Korosho hizo.

Amesema kwa msimu huu,serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa pembejeo hizo bure kwa wakulima na hawatakatwa kiasi chochote cha fedha.”Fedha zimetolewa mwaka huu wa msimu ili kusaidia wakulima kupata faida kubwa, hakuna mkulima atakaekatwa hela yeyote,”alisema

Aidha Chongolo amewataka wakulima wa zao la Korosho wenye uwezo wa kubangua hata kama Korosho kidogo wanaweza kuendelea kubangua ili kuongeza thamani katika zao hilo.

Amesema kama kuna mkulima anakorosho nyingi na anataka kubangua anaweza akabangua ila sio kuuza kwa njia za vichochoroni.”ile njia ya kuuza Korosho kwa njia ya vichochoro hata mimi sitakubali tunapaswa kusubiri minada ya ya kuuza Korosho kufunguliwa,”alisema

Chongolo amewataka wakulima hao kutojiingiza katika vichochoro vya kuuza Korosho kwa njia za vichocholoni kwani kufanya hivyo kunawafanya wanyonywe katika kupata faida ya jasho lao.

Alisema wasikubali kuingizwa vichochoro na wajanja ambao miaka ya nyuma walikuwa wakitoa fedha za kupuliza dawa mikorosho ili iwe rahisi wao kuja kuwanyonya.

“Sasa hivi mmepuliza dawa katika mikorosho yenu na mmeletewa pembejeo bure na Rais Samia Suluhu Hassan kilichobaki msubiri tu msimu wa mnada utakapozinduliwa kuuza Korosho kwa faida zaidi,”alisema na kuongeza

“Na Mwaka huu Rais Samia amesema Korosho zote zitapakizwa and katika bandari ya Mtwara na sio ya Dar es Salaam kwaajili ya kusafirishia kwani bandari hiyo ambayo imepanuliwa kwa kutumia Bilioni 100,”alisema

Aidha alisema kitendo cha kuagiza Korosho hizo kusafirishwa kwa kutumia bandari ya Mtwara ni njia mojawapo ya kuwepo kwa matokeo chanya kiuchumi.

“Wengi hamtaliona hili lakini jueni magari mengi yatafanya kazi yabkubeba Korosho kupeleka bandarini na kufanya vijana kupata ajira,”amesema

Alisema serikali imetoa kiasi hicho cha Bilioni 60 za pembejeo kwa mikoa inayolima Korosho ikiwemo mkoa wa Mtwara,Lindi ,Ruvuma na Mikoa mingine inayolima Korosho ambapo fedha hizi zilikuwa zikatwe kutoka kwa wananchi.