July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo apiga marufuku wagombea nafasi za uongozi ndani ya CCM kutohusika katika mchakato wa kutoa fomu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amepiga marufuku wagombea nafasi za uongozi ndani ya chama nchi nzima ambao ni viongozi kutohusika katika mchakato wa kutoa fomu au kusimamia uchaguzi na badala yake chama kiteue mtu mwingine wa kuusimamia ili kuweka mazingira ya haki na usawa kwenye uchaguzi.

Kauli hiyo ameitoa leo mkoani Shinyanga wakati akianza ziara yake katika mkoa huo yenye malengo matatu yakiwemo Kuhimiza Uhai wa Chama ngazi ya mashina na kuzungumza na wanachama na kukagua miradi ya maendeleo kama ilivyoahudiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025.

Chongolo ameeleza kuwa, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ndani ya chama, hivyo wagombea ambao kwa sasa ni viongozi ngazi zote hawapaswi kusimamia uchaguzi ili hali wao ni sehemu ya wagombea na kutaka wakae pembeni kuanzia mchakato wa awali wa ugawaji wa fomu, mpaka vikao vya kupitisha wagombea ili kuwepo na uchaguzi wa haki, usawa na huru kwa wagombea wote.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi, fomu zitolewe kwa wogombea wote na pale ambapo kiongozi yoyote ndani ya chama anawania nafasi ni marufuku kuhusika kwenye mchakato wa uchaguzi, wabaki kuwa wagombea kama wanachama wengine ili haki itendeke, na hii ni kwa nchi nzima,” amesema Chongolo.

Katibu Mkuu amefafanua kuwa, kama Katibu wa ngazi husika anagombea kamati ya siasa ichague mjumbe mmoja miongoni mwa wajumbe asimamie uchaguzi, na kama Kamati nzima ya siasa inagombea, ngazi ya juu iteue kiongozi mmoja asimamie uchaguzi huo ili kujiepusha na ujanja ujanja wa baadhi ya viongozi wagombea kuficha fomu kwa baadhi ya wagombea wenzao kwa maslahi yao binafsi badala ya chama.

Wakati huo huo, Chongolo, amewaonya viongozi waliopewa dhamana na chama hicho, kuacha kueneza fitina na majungu dhidi ya wengine wakati wa uchaguzi wa ndani.

Mtendaji Mkuu huyo wa CCM, amesema chama hicho kina utaratibu, Katiba, Kanuni na miongozo iliyondaliwa vizuri.

“Tatizo lililopo ni baadhi ya wanaopewa dhamana kwenye maeneo kutokutenda haki. Marufuku kwa yeyote kuineza fitina, majungu, uongo na uzushi dhidi ya wengine wakati wa uchaguzi,” amesema.

Amewataka kutenda haki, akieleza kuwa haiwezekani wakati wote tangu mwaka 2017 viongozi hao wamekuwa ndani ya CCM lakini hawakuwahi kuonywa wala kujadiliwa kwenye vikao vya maadili, iweje tuhuma hizo ziibuke sasa.

Iwapo tuhuma hizo za kweli, amehoji kwanini hazikuibuliwa wakati mwingine na hatimaye waziibue kwenye uchaguzi.

Chongolo amesema huo ni ujanja ujanja wa kukata majina na kuzalisha viongozi wasio na sifa

Katika hatua nyingine, Chongolo amesema ziara yake hiyo imelenga mambo matatu ambayo ni kuimarisha chama, kukagua miradi ya maendeleo na kuwasalimu wana-CCM.