May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yatoa taulo za kike msingi na sekondari kuunga mkono hedhi salama

Judith Ferdinand,TimesmajiraOnline,Mwanza

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM )Mkoa wa Mwanza kimetoa taulo za kike kwa shule za msingi na sekondari mkoani hapa za Ibinza, Nyamh’ongolo na Nyamadoke.Hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali na wadau wengine za kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa na hedhi salama.

Wakizungumza mara baada ya zoezi hilo la ugawaji wa taulo za kike lililofanyika shuleni Nyamh’ongolo baadhi ya wananfunzi wa shule hizo wanaeleza namna ambavyo taulo hizo za kike zitawasaidia kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kipindi cha hedhi.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Nyamh’ongolo Ester Silvano ameeleza kuwa mtoto wa kike anapokosa taulo za kike kwa ajili ya kujistiri anaweza kukaa nyumbani na kuacha kwenda shule hivyo kushindwa kuhudhuria masomo.

“Akikaa nyumbani anaweza kuja mtu akamshawishi kwa kumuambia twende ukafanye tendo fulani mimi nitakupa fedha utaweza kununua taulo za kike ‘pedi’ ataenda kufanya kitendo kile cha unyanyasaji wa kingono,”ameeleza Esther.

Ameeleza kuwa kwa msaada huo wa taulo za kike uliotolewa na Jumuiya hiyo utawasaidia kwani wengine wanatoka katika familia zenye maisha magumu hawawezi kupata fedha kwa ajili ya kununulia pedi.

Naye Mwanafunzi wa shule ya sekondari Ibinza Secilia Amosi ameeleza kuwa ameishukuru Jumuiya hiyo kwa msaada huo kwani wengine hawawezi kununua pedi kutokana na changamoto ya kipato cha familia.

Kwa upande Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Aminmohamed Velji amewahimiza wazazi kutambua wajibu wao katika kuwapatia watoto elimu ikiwa ni pamoja na kuacha tamaa ya mali.

“Ushirikiano wa wazazi na walimu ndio utaleta matunda bora kwa wototo wetu eilimu ni msingi,zile tamaa naomba niwaambie wazazi tuziache tuwasomeshe na siyo kuwaozesha wakiwa katika umri wa kusoma kwani ndio viongozi wetu wa baadae,”amesema Velji.

Hata hivyo baadhi ya vingozi wa jumuiya hiyo wanahimiza wanafunzi kuzingatia masomo pamoja na waalimu na wazazi kuwasaidia watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi kuweza kuhudhuria masomo.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi Mkoa wa Mwanza Jane Kiwala ameeleza kuwa amewataka wasikatishe masomo yao kwa kuhakikisha watoto wa kike na kiume kusoma na kumaliza masomo.

“Kama kuna changamoto yoyote kuna walimu ambao ni walezi katika shule husika nendi ukamuone msiwaogope ni kama wazazi huko nyumbani mwambie mabinti hata shuleni kuna vifaa mbalimbali ambavyo vipo kwa ajili ya kuwastili watoto wa kike,”amesema Jane.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Ilemela Michael Bahati, ameeleza kuwa wazazi wawafundishe watoto huko nyumbani kwa kuwaeleza hali halisi hasa watoto wa kike kuwa wanapoingia katika hali hii ya utu uzima madhara yake ni nini.