May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘PSSSF mnaupiga mwingi’- Majaliwa

 NA K-VSI BLOG/KHALFAN SAID, ARUSHA

MAADHIMISHO ya 3 ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, yamefunguliwa rasmi na Wazri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Novemba 22, 2023.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambao uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo Kiuchumi”, na yemelenga kutoa elimu kwa umma na hivyo kukuza uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia huduma rasmi za fedha ili kujikwamua kiuchumi na kupunguza kiwango cha umasikini nchini.

Kabla ya kutoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ili kupata maelezo ya huduma wanazotoa na miongini mwa mabanda hayo ni banda la PSSSF, ambapo alipokelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu, Mhandisi Cyprian Luhemeja na Mkurugenzi Mkuu, CPA. Hosea Kashimba.

Akitoa taarifa kwa Mhe. Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, alisema, Mfuko pamoja na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama na wananchi wanofika katika banda hilo pia unatoa elimu ya fedha.

“Mhe. Waziri Mkuu PSSSF inaingiza kwenye uchumi wa nchi kiasi cha shilingi bilioni 150 kila mwezi kama mafao ya pensheni na mafao mengine yakiwemo ya kustaafu ya mkupuo (lump sum)” Alisema.

Fedha hizi ni nyingi, elimu inahitajika ili wanaozipokea waweze kuona namna bora ya kutumia mafao hayo kwa maendeleo yao binafsi na uchumi wa taifa hili kwa ujumla.” Alifafanua CPA. Kashimba.

Aidha kuhusu ulipaji wa mafao, CPA. Kashimba alimueleza Waziri Mkuu kuwa, kwa sasa Mfuko unalipa ndani ya siku 14 baada ya mtu kustaafu na lengo ni kwamba mtu anapoondoka kazini akutane na cheki yake benki, alisisitiza.

Maelezo hayo ya CPA. Kashimba yalimfanya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kusema “PSSF mnaupiga mwingi”.

Awali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya Mifuko iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amewahimiza wananchi kutembelea mabanda yaliyo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, PSSSF, NSSF, WCF na NHIF, ili kupata elimu ya hifadhi ya jamii na elimu ya fedha.

“Mifuko yetu imewekeza katika elimu ya fedha kwa umma, haiishii kulipa mafao tu, tunatoa elimu, mfano mtu anapostaafu na kupata mafao yake tunamuwezesha kupata elimu kabla ya kustaafu, ili mafao atakayopokea yaweze kuwa endelevu na yaweze kumuhudumia katika kipindi chote cha maisha yake ya kustaafu.” Alifafanua Profesa Ndalichako.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (wapili kulia), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (wakwanza kulia), Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi. Cyprian Luhemeja, (wapili kushoto), wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (wakwanza kushoto), wakati akitoa taarifa ya mfuko katika Maadhimisho ya 3 ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Novemba 22, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (katikati), akionyesha alama ya “Dole” alipotembelea banda la PSSSF
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja (katikati) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu, PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (wapili kushoto), Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe na Meneja wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Bi. Vones Koka, nje ya banda la PSSSF.

Afisa Matekelezo, PSSSF, Bw. Erick Mremi (kushoto), akimpatia kijitabu cha Muongozo wa Mwanachama, Msanii maarufu nchini, Mrisho Mpoto “Mjomba” alipotembeela banda la PSSSF.

Afisa Usimamizi Kumbukumbu, Hellen Mbaga

Mkurugenzi Mkuu cpa. Hosea Kashimba, katika picha ya pamoja na watumishi wa PSSSF