May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijijini,Mbezi Beach B

CCM Kata Kawe yawatia kiburi wakazi Kijijini

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

BAADHI ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kawe, wamebainika kuwa kikwazo cha kuondoka kwa wakazi wa eneo la Kijijini lililopo Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kama ilivyoamuliwa na Serikali wilayani Kinondoni.

Mkuu wa Polisi Kawe(OCD) SP. Deus Shata, (wapili kushoto) akizungumza na baadhi ya wakazi wa eneo la Kijijini, lililoko Mbezi Beach B, kata ya Kawe, wilayani Kinondoni mwishoni mwa wiki. Wakazi wa eneo hilo walipewa siku 14 na Mkuu wa Wilaya hiyo kuondoka katika eneo hilo lakini wamekaidi. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Kata ya Kawe, Husna Nondo wengine ni maofisa kutoka idara mbalimbali za serikali. (Picha ya Maktaba)

Wakazi hao wa eneo la Kijijini ambako zinaishi kaya kati ya 30 hadi 40, wanatakiwa kuondoka eneo hilo baada ya kujihalalishia vitendo vya uhalifu hadharani, ikiwemo uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe haramu ya gongo na ngono za nipe nikupe.

Pamoja na wakazi hao kupewa siku 14 za kuondoka eneo hilo, ambazo zimemalizika wiki iliyopita, imebainika kwamba miongoni mwa wanaowatia kiburi ni baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Kawe, ambapo mmoja wao anaendesha biashara ya Pool Table eneo hilo.

Katika mkutano uliofanyika juzi baina yao na baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Kawe, wakazi hao walitakiwa kutoondoka eneo hilo hadi Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Kawe itakapokutana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kinondoni ili kutatua tatizo hilo.

Maelekezo hayo yaliyotolewa na kiongozi huyo wa CCM Kata ya Kawe kuwataka wasiondoke, yametafsiriwa na wakazi hao kama ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na mganga kutoka mkoani Mtwara, aliyeletwa na baadhi ya wananchi hao kwa ajili ya kuwafanyia zindiko ili wasiondoke wala kubugudhiwa.

“Kwa kweli ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya viongozi wa CCM Kata wanapingana na viongozi wa Serikali, huku ni kuwapa kiburi, CCM haijivunii wapiga kura wanaojihusisha na uhalifu,” amesema mmoja wa watoa habari wetu aliyehudhuria mkutano huo wa juzi.

Kibaya zaidi Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mbezi Beach B amepewa maelekezo ya kutowabugudhi wakazi hao, kauli ambayo inazidi kuonekana ni matokeo ya kazi iliyofanywa na mganga aliyewasili tangu Jumapili usiku na kuanza kazi yake.

Katibu wa CCM Kata ya Kawe, Aisha Katundu, akizungumza na gazeti hili jana, alisema mara baada ya kupokea kero za wanachama wa kata ya Kawe eneo la Kijijini kwamba walipewa notisi ya siku 14 na Mkuu wa Wilaya kuondoka eneo hilo, waliomba kwa uongozi wa CCM waongezewe muda.

Alisema waliomba wapewe muda kutokana na baadhi yao kuwa na vijana waliokuwa wakisoma na wamefanya mitihani ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na cha nne, hivyo wanahitaji kusubiria matokeo yao wakiwa kwenye makazi yao eneo hilo.

“Kwa hiyo sisi kama Chama tulipokea ombi lao na tunalifanyia kazi ikiwemo kuwa na mipango ya kwenda kuzungumza na mkuu wa wilaya ya Kindondoni kuhusiana na ombi lao,” amesema Katundu.

Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kawe, Othman Chipeta alisema waliongea na wakazi wa Kijijini na sasa watakwenda kuwasilisha ombi lao kwa DC kwa sababu eneo hilo wapo pia wana-CCM.

Hata hivyo, alikiri kuwa wapo wanaovuta dawa za kulevya, lakini pia wapo watu wazuri kwa hiyo Mkuu wa Wilaya ndiye mwenye maamuzi.

Katibu Mwenezi Kata ya Kawe, Yasufu Ndanga (Potipoti) alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu CCM Kata ya Kawe kuwazuia wasiondoke eneo hilo, alijibu; “Siwezi kuongea kwenye simu suala hilo.”