May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Camel Oil, Cement wakabidhi mil 100 kusaidia waathirika wa mafuriko Hanang

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KAMPUNI ya Amsons Group kupitia kampuni zake za Camel Oil na Camel Cement zimekabidhi hundi ya Sh.milioni 100 kwa Serikali kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko ya matope yaliyotokea Hanang mkoani Manyara.

Mbali na kukabidhi hundi hiyo pia Kampuni ya Camel Oil imetoa misaada mbalimbali kama Magodoro, maji na mablanketi kwa ajili ya waathirika hao na hiyo ni sehemu ya kampuni kurejesha tabasamu kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hundi ya milioni 100 pamoja na mahitaji hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa fedha na msaada huo vifaa hivyo kwa ajili ya waathirika wa mafuriko hayo.

“Tumepokea Sh.milioni 100 kutoka Camel Cement lakini na vitu vingine kutoka Camel Oil na tunaomba kwa niaba ya Serikali mtupelekee salamu kwa menejiment tunashukuru.

“Bado tunahitaji misaada ya kibinadamu ili kuwezesha ufumbuzi wa muda na wa kudumu kwa ajili ya ndugu zetu ili maisha yarejee kama kawaida ” amesema Waziri Jenista.

Awali wakati abakabidhi misaada hiyo Meneja Masoko na Uhusiano wa Umma wa Amsons Group, Bhoke Rioba amesema Camel Cement imeweka fedha kwenye akaunti ya maafa ya Serikali kiasi cha Sh.milioni 100, magodoro 100 pamoja na mashuka 100.

Amesema kutoa kwao fedha na msaada huo ni muendelezo wa kampuni hizo kwenye kampeni yake ya kurudisha tabasamu kwa jamii ya Tanzania.