April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAG apendekeza OR-TAMISEMI kuhakikisha mamlaka za serikali za mitaa zinazuia kujirudia kwa matumizi yasiyo na tija

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MTHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG)Charles Kichere amependekeza ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)ihakikishe kuwa mamlaka za serikali za mitaa zinazuia kujirudia kwa matumizi yasiyo na tija kwa kuimarisha
mfumo wa udhibiti wa ndani katika usimamizi wa matumizi,uwasilishwaji makato ya watumishi kwa wakati na kuzingatia sheria na kanuni katika kufanya uamuzi hivyo malipo kufanyike kwa shughuli halali tu.

Kupitia Ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa serikali kuu kwa mwaka wa fedha 2022/23 amesema hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya maofisa wote
wanaohusika na matumizi yasiyo na tija, ikiwamo kuripoti masuala
hayo kwa vyombo vya uchunguzi pale inapofaa.

“Nilibaini kuwa mamlaka 16 za serikali za mitaa zilifanya malipo yenye
thamani ya Sh. bilioni 1.44 kwa fedha taslimu kwa walipwaji mbalimbali,
wakiwamo wazabuni na watumishi, kinyume na takwa la mwongozo uliobainishwa,”amesema Kichere.

Amesema kufanyika kwa matumizi yasiyo na tija kunatokana na upungufu katika
mfumo wa kudhibiti matumizi hivyo kusababisha kufanya malipo zaidi ya
huduma iliyotolewa, adhabu kwa kuchelewesha malipo mbalimbali,
kutowasilishwa kwa makato ya watumishi kwa wakati, na malipo kwa
shughuli ambazo hazijatekelezwa.

“Matumizi yasiyo na tija huathiri utekelezaji wa shughuli zilizopangwa na
taasisi,”amesema.