April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAG abaini hatua za kudhibiti upungufu wa sukari nchini hazitoshelezi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MTHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG)Charles Kichere amesema amebaini kuwa hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Sukari ili kudhibiti upungufu wa sukari nchini hazitoshelezi.

Kwamba Kasi ya hatua zinazochukuliwa ili kuongeza uzalishaji wa sukari wa ndani kwa kuongeza uwekezaji wa ndani ya nchi, bado ni ndogo.

Kupitia Ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa serikali kuu kwa mwaka 2022/23 CAG amebaini kuwa, njia mbadala na za haraka za kudhibiti upungufu wa sukari ni kuagiza sukari kutoka nje kwa wakati. Hata hivyo, hazitekelezwi kikamilifu.

“Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2022/23
kiwango cha sukari kilichoingizwa kutoka nje ni kidogo licha ya kuwa
kiasi kilichoidhinishwa cha kuagiza sukari kilikuwa kikubwa kwa ajili ya
sukari ya majumbani na viwandani,

“Nina mashaka juu ya sababu za uwepo wa upungufu huu hali ya kuwa Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari nyingi zaidi kwa lengo la kudhibiti hali hii,”amesema.

Amesema Chanzo Taarifa ya bodi ya wakurugenzi Kutokuwa na udhibiti wa kutosha wa upatikanaji wa sukari sokoni
kunasababisha ongezeko kubwa la bei za sukari kusikotarajiwa ambazo
wananchi wengi hawazimudu.

Pia,amesema kunasababisha ongezeko la bei za bidhaa za viwandani ambazo zinategemea sukari wakati wa uzalishaji, hivyo kuongeza mzigo wa bei kwa watumiaji wa bidhaa hizo, ambao wengi ni wananchi wa kawaida.

“Ninapendekeza Bodi ya Sukari kwa kushirikiana na Serikali
kuhakikisha ufanisi wa usimamizi na udhibiti wa upungufu wa sukari
kwa kuhakikisha kiwango cha sukari kilichokubaliwa kuagizwa
kutoka nje kinaagizwa kwa wakati na kwa ukamilifu,kupitia na kuhakiki utekelezaji wa vibali vya uagizaji wa sukari vilivyotolea na kuchukua hatua stahiki kwa waagizaji ambao hawakutimiza
majukumu yao na kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango mikakati
ya muda mrefu ya uzalishaji wa sukari ya kutosha ndani ya nchi,”amesema CAG.