April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bonanza la michezo ya asili latumika kupinga ukatili

Na Mohamed Kazingumbe, TimesMajira Online

WANANCHI wa Kata ya Makangarawe Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam, wameapa kutofumbia macho aina yoyote ya ukatili wa kijinsia wilayani mwao.        

Tamko hilo limetolewa na wananchi hao katika Bonanza maalumu la michezo ya asili lililofanyika katika uwanja wa Makaburi ya City, Temeke mbele ya Diwani wa Kata ya Makangarawe, Morice Edward Kapinga amewakilishwa na Mwenyekiti wa Serikali wa Mtaa wa Mbonde, Rashidi Mbanga.

Bonanza hilo liliraratibiwa na Kituo cha Maendeleo na Taarifa Kwa vijana Makangarawe (Makangarawe Youth Information and Development Centre (MYIDC) lililobeba kauli mbiu ya ‘Ni wajibu wetu sote kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya Wanawake na Wanaume’.

Miongoni mwa washiriki na klabu za bao, Draft, Soka na Ngoma ya asili katika ngoma, kikundi cha Hisia Theatre Arts Group cha Temeke ambacho kilitia fola kwa mchezo wa Nyoka na Ngongoti.

Katika mchezo wa Bao, bingwa wa Taifa Ally Makosagani kutoka klabu ya Mtea alileta heshima kwa timu yake kwa kumtoa Hamidu Ally wa klabu ya Mchambwa kwa ushindi wa goli 2-0.

Katika risala yao wananchi hao wamemhakikishia Diwani na Serikali ya Wilaya ya Temeke kwamba vitendo vya ukatili na unyanyasaji umefikia kikomo kwani kufumbia macho kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kumefuga utovu wa amani katika mitaa yao.

Akiongea na wananchi hao aliwapongeza kwa kauli yao na kuwataka wawe mfano katika kata na Halmashauri ya Temeke. “Napongeza kwa kauli yenu, napenda iwe ya mfano katika Wilaya yetu”.

Wadhamini wa Bonanza hilo la michezo na Burudani Men Engage Tanzania (MET) kwa kupitia MYIDC walitoa ujumbe kuhamasisha wana makangarawe na Temeke kwa ujumla wao kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi kufungua bonanza hilo Katibu wa MYIDC, Hashimu Mohamedi Polwe amesema kumekuwa na Ukatili na unyanyasaji kwa pande zote wanaume na wanawake na watoto lakini wengi hawatoi Malalamiko kutokana wanao fanya vitendo hiyo ni wanafamilia.