April 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya REA yaridhishwa na kasi ya usambazaji umeme Mbeya

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeeleza kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya, huku ikitoa onyo kali dhidi ya hujuma na wizi wa miundombinu ya nishati hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi katika Kitongoji cha Iwambi, Halmashauri ya Mbeya Vijijini , Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Florian Haule, amewataka wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa vifaa vya umeme vikiwemo mashine umba (Transfoma) na nyaya zake.

“Uharibifu au wizi wa vifaa hivi husababisha hasara kubwa kwa Serikali na kuchelewesha huduma kwa wananchi. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu hii inalindwa ili kuleta tija iliyokusudiwa,” amesema Haule.

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.9 unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO). Kwa mujibu wa Mhandisi Abdallah Mitenda kutoka ETDCO, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei 2026, ikiwa ni mapema zaidi ya muda wa mkataba uliopangwa awali.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Mhandisi Ajuaye Jeggo, amewahimiza wananchi katika maeneo hayo kukamilisha zoezi la kusuka waya kwenye nyumba zao (Wiring) ili waunganishwe na huduma hiyo kwa gharama nafuu ya Shilingi 27,000 tu. Takribani wateja 3,465 wanatarajiwa kunufaika na mradi huu ambao unahusisha ufungaji wa transfoma 105 na ujenzi wa laini za umeme zenye urefu wa kilomita 210.

Awali; Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo amewapongeza Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali akisema ni hatua muhimu ili kuhakikisha Miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.

“Ufuatiliaji na ukaguzi wa Miradi unasaidia kuongeza uwajibikaji kwa wataalam na wakandarasi; hali hiyo inasaidia wananchi wanapata huduma bora kama ilivyokusudiwa na Serikali,” amesema Mpogolo.