April 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajumbe wa Bodi ya REA waipongeza ETDCO

Na Mwandishi wetu.timesmajira

WAJUMBE wa Bodi ya Nishati Vijijini Vijijini (REA) wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 10.9 za Kitanzania unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO).

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Abdallah Mitenda, amesema kuwa Kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha mradi unakamilika mwishoni mwa Mei 2026, hivyo kukamilika ndani ya mwaka mmoja badala ya miaka miwili kama iliyopangwa kwenye mkataba.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka ETDCO, Mhandisi Ajuaye Jeggo, amesema kuwa kupitia mradi huo wanatarajia kuunganisha wateja takribani 3,465, huku akitoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayofikiwa na mradi huo kwa kufanya maandalizi ya ndani ya nyumba ( wiring) ili waweze kuunganishiwa umeme mara moja pindi huduma itakapoanza kwa gharama ya shilingi 27,000

Nao, wananchi Mkoa wa Mbeya, wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini kwa kuwaletea mradi huo kwani utasiadia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao.

Mradi huo unaotekelezwa na ETDCO unahusisha ujenzi wa laini ya umeme ya msongo wa kati yenye urefu wa takribani kilomita 1.5, laini ya msongo mdogo yenye urefu wa kilomita 210 pamoja na uwekaji wa mashine umba (Transformer) 105.