April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko asisitiza msimano wa Rais Samia kwa wafanyabiashara

Na Mwandisha Wetu,TimesmajiraOnline, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kama mlezi wa Sekta
binafsi nchini na hataki kuona wafanyabiashara wanapata misukosukowakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema maono ya Rais ni kujenga sekta binafsi itakayokuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa na ili kufikia azma hiyo, viongozi wengine wahakikishe nia njema ya Rais kwa Wafanyabiashara inatekelezwa kwa vitendo.

Dkt. Biteko amesema hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Rafiki Hoteli ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Aidha, Dkt. Biteko amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha
wanailea Sekta binafsi na kila mtu atimize wajibu wake kwenye eneo
lake “kama wewe ni Afisa wa TANESCO uliye na wajibu wa kumuunganishia mfanyabiashara umeme ambao mwisho wa siku ataulipia kwa ajili ya mapato yako, huna sababu ya kumwambia njoo kesho wakati kazi hiyo ungeifanya leo.”

Amesema Watendaji ambao ni warasimu lazima waone aibu kwa kuchelewesha shughuli zinazoijenga nchi.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka kuona Watanzania wakiwa kwenye daraja la kwanza katika nchi yao na pia waweze kufanya uwekezaji ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

Kuhusu Sekta ya Utalii nchini, amesema bado kuna changamoto ya
upungufu wa vitanda kwa wageni wa ndani na nje ya nchi hivyo bado kuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya hospitality ambapo
amewapongeza wamiliki wa Rafiki hoteli na wawekezaji wengine ambao
wanaifanyia kazi changamoto hiyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
(katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Rafiki Hoteli iliyopo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu na Mmiliki wa Rafiki Hoteli, Fladmiry Mallya.

Vilevile, Dkt. Biteko ameipongeza menejimenti ya hoteli hiyo kwa
kutekeleza dhana ya nishati safi ya kupikia kutokana na kuweka
miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye hoteli husika na kutoa wito kwa wananchi kutoharibu mazingira na kutokukata miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu Idara na
taasisi mbalimbali Serikalini kutumia miundombinu ya uwekezaji Jijini Dodoma ambayo ndio Makao Makuu ya Nchi.

Kutokana na hilo ameagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha kwamba
shughuli zinazoweza kufanyika ndani ya Mkoa wa Dodoma zifanyike katika Mkoa husika ili pia kutoa fursa kwa wanachi kupata huduma muda wote pale wanapohitaji huduma za watendaji hao.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mmiliki wa Rafiki Hoteli Fladmiry Mallya ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanafanya Watanzania kuendelea kuwekeza kwenye nchi yao na hivyo kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira.