May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 25.3 zaboresha barabara Musoma

Na Mwandishi Wetu, TimeMajira Online

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 25.3 zimetumika kuboresha barabara na mitaa ya Manispaa ya Musoma ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka 2015 -2020.

Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 18.7 zimetumika kujenga kilometa 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika.

Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wakazi wa mji wa Musoma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Mara Sekondari, Kata ya Nyamatare, Wilayani Musoma.

Amesema, kupitia Road Fund (Maintenance) kiasi kingine cha Sh. bilioni 6.6 kilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na kwamba miradi yote imekamilika.

Majaliwa ambaye yuko Mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini, Vedasto Manyinyi, mgombea udiwani Kata ya Nyamatare, Masumbuko Magesa na madiwani wengine wa manispaa hiyo.

“Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura Dkt. Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu,” amesema.

Akielezea mambo mengine yaliyotekelezwa chini ya Ilani hiyo, Waziri Majaliwa amesema, kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani iliyolenga kumpunguzia mama kazi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji imefanikiwa kwa asilimia kubwa na kwa sasa katika maeneo mengi wanatembea hatua chache kutoka bombani hadi nyumbani akiwa ameshika ndoo yake mkononi.

“Ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwenye mji wa Musoma, shilingi bilioni 46 zilitolewa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi katika Manispaa ya Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma,”.

Amesema, sh. bilioni 18 zimetolewa kwa mradi wa kusambaza maji katika Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini na Butiama, ambapo kazi zinazofanywa ni ujenzi wa tenki la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (Booster station) na ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kwenda kwenye tenki la Bharima (Rising main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56.

Kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kwenye tenki la Bharima kwenda kwa wananchi (Transmission main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7.058; ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa; ununuzi ya bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.