May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biashara haramu ya sigara hatari kwa usalama wa nchi

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

WADAU wa maendeleo Mkoani Songwe wametakiwa kuunganisha nguvu kwa pamoja katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya Sigara ili kulinda mapato ya serikali na afya ya umma, ikiwemo kuimarisha amani na usalama wa Taifa.

Rai hiyo, imetolewa leo,Aprili 19, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja ya kujadili biashara haramu ya sigara kwa wadau wa maendeleo iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Kampuni ya sigara Tanzania (TCC) na ofisi ya Mkuu ya Mkoa.

Mgomi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo katika kikao hicho, amesema kuwa matokeo hasi yatakayotokea ikiwa biashara haramu ya sigara na bidhaa za magendo itaachwa bila uangalizi ni hatari kwa uchumi na usalama wa nchi kwa kuwa ndio biashara kubwa ya pili baada ya dawa za kulevya kwa mapato yatokanayo na magendo.

“Tunajua kuwa kuwepo kwa sigara za magendo na soko haramu husababisha ukwepaji kodi kwani mapato hayo yanayopotea yangeweza kutumika katika kuboresha utoaji wa huduma za umma kama vile afya, elimu na miundombinu” amefafanua Mgomi.

Amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa faida itokanayo na biashara haramu ya sigara mara nyingi huishia kwenye mifuko ya mashirika ya kihalifu na hivyo kuchochea shughuli nyingine haramu na kuhatarisha usalama wa nchi.

Aidha, Magomi amesema kuna tishio la kiafya kwa umma linalosababishwa na biashara haramu ya sigara bandia ambazo hazina viwango vya usalama kwa kuwa mara nyingi zimekuwa na viambata hatari visivyokubalika katika kanuni za afya.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, ameitaka kampuni ya sigara Tanzania kuendelea kutoa elimu kwa jamii hadi ngazi za chini ili kujenga uelewa juu ya bidhaa bandia na magendo, ikiwemo kushirikisa kamati za usalama za wilaya ili kudhibiti wimmbi la biashara haramu hasa maeneo ya mpakani.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya sigara Tanzania (TCC), Takahashi Araki, licha ya kampuni hiyo kuwa mlipaji mkubwa wa kodi za serikali, kampuni imekuwa ikikabiliana na changamoto kubwa katika soko kutokana na uingizwaji mkubwa wa sigara haramu na bidhaa za magendo.

Araki amesema katika kipindi cha mwaka wa 2023 kampuni ya sigara Tanzania iliongeza hali ya uzalishaji wa sigara nchini kwa kuzalisha sigara bilioni 6.5 na kulipa kodi ya serikali kiasi cha shilingi 325.9 bilioni.

Mkurugenzi wa uhusiano na mawasiliano wa kampuni ya sigara Tanzania, Patrcia Mhondo, amesema lengo la warsha hiyo ni wadau wa maendeleo kukutana na kuweka mikakati ya pamoja ya kumaliza tatizo hilo la biashara haramu ya sigara na bidhaa za magendo hususani katika maeneo ya mpakani.